Na Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) inatarajia
kuanza kambi rasmi wiki ijayo ili kujiandaa na mashindano yajao ya Shirikisho
la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika
kitaifa mkoani Iringa.
Mwenyekiti wa Timu hiyo Wilson Dede amewataka
wanamichezo wote kutoka Mikoa yote nchini kufika katika Viwanja vya Shule ya
Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) kwa ajili ya kuanza mazoezi kuelekea mashindano hayo.
“Wanamichezo wote wanatakiwa wawe Dar es Salaam
kuanzia tarehe 22 Septemba, 2023, tayari kwa ajili ya kuanza mazoezi ya pamoja
ili kumpa nafasi mwalimu kuchagua kikosi imara kitakachopeperusha vyema bendera
ya Mahakama ya Tanzania SHIMIWI...
“.....nadhani unajua kilichotokea Tanga, tutaanzia tulipoishia
mwaka jana na tutapiga pale pale kwenye mshono. Ndiyo maana tumeamua kuanza
kambi mapema ili tuweze kuunda timu imara yenye ushindani katika michezo yote
tutakayoshiriki,” alisema.
Michezo ambayo Mahakama Sports inatarajia kushiriki ni
Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata,
Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Mwenyekiti wa Timu ya Tanzania (Mahakama Sports), Wilson Dede akieleza utaratibu wa mazoezi utakavyokuwa katika Viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni