Jumamosi, 16 Septemba 2023

WATUMISHI MAHAKAMA KIGOMA WAFURAHISHWA NA UTEUZI WA JAJI MLACHA KUWA JAJI RUFANI

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephano Magoiga, ameongoza watumishi wa Kanda hiyo kushangilia na kumpongeza aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Lameck Mlacha kufuatia kuteuliwa kwake na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Akizungumza mara baada ya hafla ya uapisho tarehe 14 Septemba, 2023, Mhe. Magoiga, alisema Kanda ya Kigoma wanamshukuru Mungu kwa Mamlaka ya uteuzi ya Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini Jaji Mlacha kuendelea kulitumikia Taifa katika ngazi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Jaji Magoiga pamoja na sehemu ya watumishi wa Kanda hiyo waliokuwa wakifuatilia hafla ya uapisho iliyokuwa ikirushwa mubashara kwa njia ya Runinga alisema, “tunamtakia heri katika majukumu yake mapya hekima za Mungu zikawe pamoja nae na wenzake.”

Jaji Mlacha ni miongoni mwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wanne (4) na wa Mahakama Kuu 20 walioteuliwa tarehe 03 Septemba, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuapishwa tarehe 14 Septemba, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakifuatilia hafla ya uapisho wa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu iliyokuwa ikirushwa mubashara kwa njia ya Runinga tarehe 14 Septemba, 2023, hafla hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Stephano Magoiga akifuatilia hafla ya uapisho wa Majaji wapya kwenye runinga akiwa ofisini kwake Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.
Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni