Ijumaa, 15 Septemba 2023

WCF NA MAHAKAMA YA KAZI YAENDESHA MAFUNZO KWA MAJAJI, WASAJILI KANDA YA ZIWA

Na. Stephen kapiga - Mahakama Mwanza.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kushirikia na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wameanza kuendesha mafunzo kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Manaibu Wasajili wa Kanda za Mwanza, Bukoba, Musoma na Shinyanga kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutafsiri sheria za kazi na Fidia kwa wafanyakazi wenye migogoro yenye asili ya kazi.

Akifungua kikao hicho kilichoambatana na mafunzo hayo ya umahiri wa kutafsiri sheria za kazi leo tarehe 15 Septemba, 2023 jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dkt. John Mduma aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano inaoutoa katika kufanikisha mafunzo hayo kwa Majaji na Mahakimu tangu yalipoonza kwa mara ya kwanza June 9 hadi 10 huko wilayani bagamoyo.

“kwa mwaka 2018 mfuko ulifanya mafunzo kama haya kwa Mahakimu 80 ya kuwajengea uwezo katika majukumu yao ili kuwezesha kuwasaidia wanaostahili kupata fidia zao wapate kwa wakati. Kwa siku ya leo lengo la mafunzo haya ni kuwapatia washiriki wanaoshiriki mafunzo haya uelewa wa sheria mbalimbali zinazohusu fidia kwa wafanyakazi” alisema Dkt John Mduma.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alimshukuru Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa utayari wake wa kushirikiana na Mahakama ili kukiwezesha Kitengo cha Kazi katika kutimiza majukumu yake la kutoa haki kwa wananchi kwa weledi na umahiri mkubwa.

“Baada ya kuhamia Dar es salaam kama Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi nilifanya ziara ofsini kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nikiwa na lengo la kujitambulisha na kuona namna bora ya kuweza kushirikiana na Mfuko ili kupanga mikakati ya kuona namna bora ya kushirikiana katika kutimiza Nguzo ya tatu (3) ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025 kwa kushirikina na wadau wengine” alisema Dkt. Yose Mlyambina 

Mhe. Mlyambina amesema, Mafunzo hayo yatawajumuisha Majaji kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Divesheni ya Kazi, Majaji Wafawidhi kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Musoma na Kagera pamoja na Majaji kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza. Vilevile Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hizo. Wengine wanaoshiriki mafunzo hayo ni Maofisa kutoka Tume ya Usuluhishi (CMA) na Maafisa mbalimbali kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. 

Tangu kuanza kwa mashirikiano hayo na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Mahakama ya Tanzania Divisheni ya Kazi kumekuwa na tija kubwa kwani mpaka sasa mfuko huo umeweza kuiwezesha Mahakama ya Kazi Maktaba ya Divisheni hiyo mjumuisho wa sheria za kazi katika nakala laini na ngumu na pia kutoa komputa mpakato na desktop kwa Divisheni hiyo kwa ajili matumizi ya Makataba ya Divisheni ya Kazi.

Kikao hicho kitafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo tarehe 15 septemba, 2023 hadi tarehe 16 septemba, 2023 ambapo kikao kazi hiki kitafungwa rasmi kwa Kanda ya Ziwa na kuelekea Kanda zingine.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akitoa salamu kutoka Mahakama ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo kilichoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kushirikia na Mahakama ya Tanzania mafunzo yanafanyika jijini Mwanza kwa muda wa siku mbili.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dkt. John Mduma akitoa neno la ufunguzi wakati wa ufungiaji wa mafunzo yanayohusu Sheria za Fidia kwa wafanyakazi yaliyoandaliwa na Mfuko huo jijini Mwanza.

Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda za Mwanza, Shinyanga, Bukoba na Musoma wakiwa kwenye picha ya pamoja na Meza Kuu.


Sehemu ya Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kanda ya Ziwa wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu




(Stori hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni