Na. Faustine Kapama-Mahakama na Sade Soka-UDSM
Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana leo tarehe 15 Septemba, 2023 amemtembelea
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar
es Salaam na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa kuiheshimisha Tanzania kimataifa.
Mhe.
Balozi Chana, ambaye aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul na
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara hiyo, Bw. Abdulrahman
Mshamu, amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambayo masuala ya utawala wa Sheria
yanazingatiwa.
“Tunapata
fursa wakati mwingine kwenda Nchi mbalimbali, ukuenda huko duniani ndipo utakapojua
kwamba Tanzania tupo vizuri. Niliwahi kwenda (sehemu) nikaambiwa hapa hakuna
Bunge, Mahakama haieleweki, kwa kweli sisi tupo mbali. Mhimili wa Mahakama
unatuheshimisha kama Taifa, tunakupongeza sana,” Waziri Chana alimwambia Jaji
Mkuu.
Ameeleza
dhumuni la kumtembelea ni kujitambulisha na kujifunza mambo mbalimbali
yanayofanyika katika Wizara yake, kama alivyofanya kwenye taasisi zingine,
ikiwemo Shule ya Sheria kwa Vitendo na kuahidi kushirikiana na Mahakama
kushughulikia mambo kadhaa ya kiutendaji yanayoikabili Shule hiyo.
“Tunawakuomba
sana msiache kutushauri kuhusu suala hili la Shule ya Sheria kwa Vitendo, nyinyi
mmebobea kwenye vyuo hivi, mnaweza kushauri tuboreshe wapi, haiwezekani kwa
nini watu walalamike kuwa hawafaulu kwenye masomo yao. Milango yetu ipo wazi, mkitaka
maboresho ya bajeti, sheria na kanuni, haya ni majukumu yetu, sisi tutakuwa tayari
muda wowote,” amesema.
Naye
Naibu Waziri amemshukuru Jaji Mkuu kwa
kuimarisha utendaji katika Mahakama ya Tanzania kwani picha iliyopo huko nje,
hasa katika Magereza, ni nzuri kwani wafungwa na mahabusu wanaridhishwa na kasi
ya usikilizaji wa mashauri yao.
“Picha iliyoko huko ni
nzuri kwa kweli, tumekuwa tukitembelea Magereza tunakutana na mahabusu na
wafungwa, wanawapongeza sana na wamefurahi namna wanavyo angaliwa vizuri na
Mahakama, nakala zao za hukumu wanazipata kwa wakati, kesi zinasikilizwa, hivyo
wanaishukuru Mahakama kwa kazi hii nzuri,” amesema.
Kadharika, amemshukuri
Mhe. Prof. Juma kwa kuwawezesha kama Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kujionea
miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama, hatua inayomsaidia kujibu kwa ufasaha
maswali anayokutana nayo bungeni.
“Naupongeza Uongozi wa
Mahakama kwa kushirikiana nami na kuwa tayari kunisaidia katika hatua
mbalimbali, ikiwemo kujibu maswali ninayoyapata bungeni, hasa suala hili la miradi
inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60,” amesema.
Akizungumza
na wageni wake, Jaji Mkuu alimpongeza Waziri Chana kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na Mhimili wa
Mahakama. Amemkaribisha kuitembelea Mahakama mara kwa mara ili kujifunza
shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mhimili huo.
“Kuna
maeneo ambayo yanasukuma maboresho ya Mahakama. Kitengo cha Maboresho ni Injini,
haya maboresho yanayoendelea kuna watu ambao wapo masaa 24 wakiangalia kitu
gani kipo wapo, majengo yakoje, TEHAMA ipo vipi, tuna Kituo Jumuishi cha
Masuala ya Familia, ni Dunia nyingine kabisa. Hivyo, haya ni maeneo ambayo ni
muhimu sana ukiyaelewa,” Mhe. Prof. Juma amemweleza Waziri Chana.
Jaji
Mkuu amemshukuru Waziri kwa kuendelea kuiongelea Mahakama katika maeneo
mbalimbali, ikiwemo Bungeni kwa kuzingatia mambo mengi yanayofanyika
hayafahamiki kwa umma kwa kiwango cha kuridhisha. “Ukisoma kwenye magazeti
kuhusu Mahakama au Wizara utashangaa kama hao wanaoandika wanaishi Tanzania.
Nadhani tunajukumu la kuuhabarisha umma,” amesema.
Kuhusu
Shule ya Sheria kwa Vitendo, Mhe. Prof. Juma amekubaliana na Waziri kuwa ni
eneo ambalo wanahitaji kulifanyia kazi kwa kushirikisha Wizara na Mahakama kwa
pamoja ili kutafuta nanma ya kutatua changamoto zinazoibuliwa, hasa katika
kuimarisha elimu kwa vitendo kwa wanafunzi.
Kwa
upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed
Siyani amesema Mahakama imekuwa ikishirikiana na Shule ya Sheria kwa Vitendo katika
kufanya maboresho na kuanzia Januari mwakani wanatarajia kutakuwa na mitaala
mipya, hatua ambayo itasaidia kubadilisha hali ya Shule hiyo.
“Toka
mwanzo ilionekana elimu iliyokuwa inatolewa ilikuwa nadhalia zaidi, ile practical aspect ambayo inatarajiwa wanafunzi
wanapokuwa katika hatua za mwisho kabisa za kuhitimu taaluma yao waipate ilikuwa
changamoto. Kwa hiyo, Mahakama imeshiriki kwenye maboresho makubwa,”
amebainisha.
Jaji
Kiongozi ameshukuru mtazamo wa Wizara kuhusu Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto kwani ni rahisi zaidi baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama
kitakuwa moja kwa moja chini ya Mahakama, hatua ambayo itaimarisha zaidi
utendaji wake.
Akizunguza katika hatika tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alimfahamisha Waziri maeneo manne ambayo wanaweza kuyatembelea, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Mteja Kinondoni, Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara.
Tukio hilo limehudhuriwa pia na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda na Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei (Ajira na Uteuzi) na Bi. Alesia Mbuya (Nidhamu na Maadili).
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana akizungumza jambo leo tarehe 15 Septemba, 2023 wakati alipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma,(hayupo katika picha) kwenye ofisi yake iliyopo jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akizungumza na mgeni wake (hayupo kwenye picha).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akisisitiza jambo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul akifafanua jambo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza mambo mbalimbali
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Abdulrahman Mshamu akizungumza kwenye tukio hilo.
Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakifuatilia kile kilichokuwa kinaendelea. Kushoto ni Bi. Enziel Mtei (Ajira na Uteuzi) na Bi. Alesia Mbuya (Nidhamu na Maadili).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana ( kushoto) na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pauline Gekul (kulia).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana (wa pili kushoto). Wengine ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kulia), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana (wa nne kushoto). Wengine ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pauline Gekul (wa nne kulia), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa tatu kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kulia),Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama-Ajira na Uteuzi, Bi. Enziel Mtei (wa pili kushoto), Katibu Msaidizi wa Tume hiyo – Nidhamu na Maadili, Bi. Alesia Mbuya ( wa kwanza kushoto) na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. SylvesterKainda (wa kwanza kulia).
HAKIMUNGEA NA MAHAKAMA YA WILAYA YA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni