- Asisitiza Maadili na Uadilifu kama
njia ya msingi wa kutekeleza jukumu la utoaji haki.
Na. Innocent Kansha – Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amesisitiza maadili
na uadilifu kwa Majaji Wapya wa Mahakama Kuu, kama njia kuu ya msingi ya kutekeleza
jukumu mama la utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza
katika kikao kilichofanyika jana tarehe 14 Septemba, 2023 Mahakama Kuu jijini
Dar es salaam kilichojumuisha Majaji wapya wa Mahakama Kuu mara baada ya kuapishwa, Mhe. Siyani alisema, majukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu yatabadilisha
baadhi ya mambo ya msingi waliyoyazoea na kwamba wameanza safari mpya ya
utumishi ambayo awali hawakuwa nayo.
“Nafahamu
kwamba baadhi yenu mmeingia kwenye utumishi wa umma kwa mara ya kwanza, lakini
pia wapo baadhi yenu ambao mlikuwa watumishi wa umma na wengine mlikuwa Maafisa
Mahakama kabla ya kupata uteuzi na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu,” alisema
Jaji Kiongozi.
Mhe.
Siyani alikumbusha kuwa, jambo la muhimu ni kwamba Mahakama ni familia moja
yenye mila na desturi moja, hivyo ni wajibu wenu kujifunza na kuzielewa kwa
haraka mila na desturi zilizoainishwa katika Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama
(The Code of Conduct and Ethics). Kwa hiyo, kila mmoja
anapaswa kufahamu dira na dhima ya Mahakama, kanuni, taratibu na miongozo
mbalimbali katika utendaji kazi.
“Mtapaswa
kujifunza tamaduni mbalimbali ambazo hazijaandikwa na kuzitafsiri ili kuboresha
mtizamo na kuleta tija katika utoaji haki, mtalazimika kuzingatia maadili
yasiyo na mashaka ili kulinda heshima ya ofisi ya Jaji wa Mahakama Kuu. Ni
muhimu kwa mfano kila Jaji kuheshimiana na mwenzake, ikiwa ni pamoja na
kuheshimu ngazi za madaraka yenu”, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Aidha,
kwa upande wa utoaji haki, Jaji Kiongozi aliwakumbusha Majaji hao jukumu la
msingi la Mahakama kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa
ni kutenda haki kwa
wote bila ya
kujali hali ya
mtu kijamii au kiuchumi, kutochelewesha haki bila sababu ya
kimsingi. Kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya
watu wengine, na kwa mujibu
wa sheria mahususi iliyotungwana Bunge na kukuza na kuendeleza
usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro.
“Tumieni
weledi na umahiri wenu, kuhakisha haki haichelewi, haipotei kwa sababu za
kiufundi, waathirika wanapata fidia inayostahili na pia kumaliza mashauri kwa
kuhimiza usuluhishi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Aidha ni vema kujifunza
mazingira ya kijamii na kiuchumi ili iwasaidie katika kujibu matarajio halali
ya wananchi wanaofika mbele yenu”, aliongeza Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi alisema, tafsiri
za sheria zijielekeze katika ustawi wa jamii ya watanzania kiuchumi na kijamii.
Hii ni kwa kuzingatia kama alivyowahi kusema Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Juma
kwamba, “Wananchi kupitia Katiba wametupa sisi Majaji
mamlaka ya utoaji haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi”
Jaji Siyani alieleza kuwa, ni
vema Majaji hao wakafahamu wakati wote, kwamba kutotekeleza jukumu la utoaji
haki kwa ufanisi, uaminifu na weledi wa kutosha, itaathiri siyo tu imani kwao bali
kwa Mahakama na mfumo mzima wa utoaji haki, kwa kuwa maamuzi yao yatatumika kama
rejea na Mahakama za chini hivyo kwa kujitahidi kutoa tafsiri sahihi inayoakisi
uzito wa dhamana ambayo Mahakama imepewa.
Alikadhalika, Mhe. Siyani
aliwahimiza Waheshimiwa Majaji kuwa, wao ni viongozi, na kwamba uongozi wao utajionyesha
zaidi katika usimamiaji na uendeshaji wa mashauri. Aidha, kwa kuwa utoaji haki unahusisha
pia wadau, onesheni mwelekeo wa utendaji utakaopaswa kuheshimiwa na wadau bila
malalamiko.
“Mna wajibu wa kusaidiana na waheshimiwa Majaji na viongozi wengine mtakaowakuta kituoni kuwaongoza na kuwaelekeza waheshimiwa Mahakimu na watumishi wengine kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi mkubwa kwa faida ya mwananchi tunayemhudumia”, alisistiza Jaji Kiongozi.
Kwa upande wa usikilizwaji wa mashauri, Jaji Kiongozi akawaomba Majaji hao kwa msisitizo kutokubaliana na suala la mlundikano wa mashauri mahakamani, kwani mashauri yenye umri unaozidi miezi 24 Mahakamani yatahesabika kama mashauri yenye mlundikano.
“Kuna
mambo mengi yanayosababisha mlundikano wa mashauri lakini kubwa zaidi ni maahirisho ya mashauri yasiyo
kuwa na sababu
za msingi. Maahirisho haya yamekuwa sababu
ya malalamiko dhidi
ya Mahakama. Suala muhimu ni
kwa kila Jaji kuwa makini na shajara au diary yake. Hakikisha kila shauri lililo mbele yako linapangiwa muda wake maalumu
ili kuepusha malalamiko yasiyokuwa ya lazima ya wadaawa kusubiri muda mrefu Mahakamani”, aliongeza Jaji
Siyani.
Mhe,
Siyani akawakumbusha Majaji hao kuendeleza jitihada za matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano alisema, kwa sasa Mahakama imejikita katika matumizi
makubwa ya TEHAMA kwenye usimamizi na
uendeshaji wa mashauri na shughuli nyingine
za utawala. Mifumo ya kielektroniki
ndiyo inayotumika katika usajili wa mashauri mahakamani, usimamizi na uhifadhi
wa kumbukumbu mbalimbali za
mashauri mahakamani kupitia mfumo wa JSDS
II na usikilizaji wa mashauri kupitia Mahakama Mtandao (video conference).
Pia
mfumo wa kuratibu taarifa za mawakili
(e wakili), vilevile Mahakama inatarajia kuhamia kwenye mfumo wa ki-elektroniki wa usimamizi wa mashauri (e – Case Management
System) ambao utatumika kusikiliza mashauri ikiwa ni hatua muhimu kuelekea Mahakama
Mtandao.
“Niwafahamishe
kuwa nanyi mtanufaika na mafunzo ya
mfumo huo. Mfumo huu unakwenda sambamba na mfumo wa kurekodi na kutafsiri (Transcription and Translation System
– TTS). Aidha,
mfumo wa ki-elektroniki wa utambuzi wa mahitaji ya Mahakama (court mapping)
husaidia kupata taarifa za majengo ya Mahakama. Hivi sasa unajengwa
mfumo wa kuratibu
taarifa za madalali
wa Mahakama”, alifafanua Mhe.
Siyani.
Jaji
Kiongozi akawahimiza Majaji hao kuwa watumiaji na vinara wa usimamizi wakuu
wa mifumo hiyo ya TEHAMA.
Lengo liwe kuhakikisha kwamba, mashauri yatakayokuja mbele yao yawe yamesajiliwa katika mfumo na taarifa zake ni sahihi, maamuzi watakayotoa yawekwe wazi
kwa umma kupitia mtandao wa TanzLII.
Vilevile
kwa kadri inavyowezekana kuwasaidia wadaawa na mashahidi wanapata nafuu ya gharama na muda kwa kusikilizwa
mashauri yao kwa njia ya mtandao
(video/audio Conferencing) bila kulazimika kusafiri kuja mahakamani, Kutumia
ipasavyo fursa ya maktaba mtandao kujifunza kwa nia ya kuimarisha weledi katika kazi zao
na kuhakikisha wanatoa mchango wao kuimarisha matumizi
ya Mahakama mtandao.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akizungumza na Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania (hawapo pichani) alipokutana nao na kufanya kikao cha pamoja ili kukumbusha baadhi ya mambo ya kiutendaji jana tarehe 14 Septemba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es salaam, wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) na (kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Mhe. Latifa Mansoor.
Sehemu ya Majaji Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakinukuu baadhi ya mambo muhimu yaliyotokana na kikao hicho cha pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo pichani)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni