·Majaji, Mahakimu wafurika kwenye Bonanza
·Usiwachukulie poa, walichokifanya Gymkhana hatari
·Jaji Maruma kumbe naye yumo
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Wanachama wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Tawi la Dar-es-Salaam leo tarehe 9 Septemba, 2023
wameshiriki katika Bonanza la Michezo mbalimbali ambalo limefana kwa kiasi
kikubwa kinyume na matarajio.
Majaji, Mahakimu na
watumishi wengine wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar-es-Salaam
walianza kuwasilisha katika Viwanja vya Gymkhana mapema asubuhi ili kushiriki katika
Bonanza hilo ambalo ni la kwanza tangu chama hicho kuanzishwe.
Dalili za kuchangamka kwa
Bonanza hilo zilianza kuonekana baada ya mgeni rasmi, Jaji na Mlezi wa
Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija kuungana na wanachama
hao na kuanza pasha-pasha ya hapa na pale kabla ya kwenda kwenye mapumziko
mafupi.
Baadaye, washiriki wa
Bonanza hilo walijigawa katika makundi ya michezo mbalimbali ambapo kila mmoja
alichangamkia nafasi yake, huku Majaji kutoka Mahakama Kuu na Mahakama ya
Rufani wakionyesha umahiri mkubwa uliowashangaza wengi.
Michezo waliyoshiriki ni
kukimbia mita 100 kwa wanawake na wanaume, kukimbia mita 400 kwa Wanawake na
Wanaume, karata, draft, bao, kukimbiza kuku, mpira wa miguu na mpira wa pete,
kuvuta kamba na kukimbia kwenye magunia.
Katika mchezo wa kukimbia
mita 100 wanawake, Mhe. Barke Sehel wa Mahakama ya Rufani aliwatimulia vumbi
wenzie, huku Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar-es-Salaam, Mhe. Sudi Fimbo akikiwasha kisawasawa. Mshindi wa mbio hizo
alikuwa Grace Hamis wa Mahakama Kuu.
Kwa upande wa mbio mita
100 wanaume, Majaji Sam Rumanyika na Zepharine Galeba wa Mahakama ya Rufani na
Majaji Edwin Kakolaki, Musa Pomo na Gabriel Malata wa Mahakama Kuu ya Tanzania walitoa
upinzani wa kufa mtu. Mshindi wa mbio hizo alikuwa Girshot Gentro kutoka Mahakama
Kuu.
Katika mbio za mita 400
wanaume, Majaji wa Mahakama ya Rufani pia hawakuwa nyuma baada ya kuwahenyesha
washiriki wengine. Mshindi wa mbio hizo alikuwa Sachore Adolfi kutoka Mahakama
ya Rufani, huku upande wa wanawake, Grace Hamis aliibuka mshindi kutokea
Mahakama Kuu.
Kwenye mchezo wa kukimbia
kwa kutumia magunia, Aziza Mnete wa Mahakama ya Rufani aliibuka mshindi, huku upande
wa wanaume, Mhe. Hassan Chuka, pia kutoka Mahakama ya Rufani akichomoza kama mbabe.
Kwa upande wa kukimbiza
kuku wanaume, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe.
Dkt. Yose Mlyambina alifanikiwa kujinyakulia kitoweo hicho, huku Naibu Msajili
Mahakama ya Rufani, Mhe. Sekela Mwaiseje akiibuka mshindi kwa upande wa
wanawake.
Katika mchezo wa
kuendesha baiskeli, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sam Rumanyika alifanikiwa
kuchanja mbuga kwa upande wa wanaume, huku Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya
Ilala, Mhe. Suzan Kihawa akiibuka kidedea.
Kuhusu kamba
wanawake, Mahakama Kuu waliwakamua kamasi Mahakama ya Rufani na kwa upande
wa wanaume Mahakama ya Rufani iliwapigisha chafya Mahakama Kuu. Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani walishiriki kikamilifu na kuonyesha
ukakamavu wa hali ya juu ambao wengi hawakuamini kilichokuwa kinatokea.
Katika mchezo wa bao, kulikuwepo
na mechi za utangulizi ambapo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs
Mwambegele alimgalagaza mtu baada ya kuibuka mshindi, huku Kaimu Mtendaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Division ya Kazi, Jumanne Muna akimsambaratisha jamaa
mmoja aliyejaribu kujitutumua.
Mchezo huo katika mashindano
ulimuibua Mwanabibi Bakari kutoka Mahakama Kuu, ambaye alimpigisha chafya mshindani
wake kutoka Mahakama ya Rufani na kwa upande wa wanaume, Hashim Rashid pia wa
Mahakama Kuu aliibuka mshindi.
Katika mchezo wa mpira wa
miguu wanaume, Timu ya Mahakama Kuu iliwachapa Mahakama ya Rufani mabao 2:1
kufuatia kabumbu safi iliyoonyeshwa na wachezaji wa timu zote mbili.
Mahakama Kuu walikuwa wa kwanza kuliona lango la wapinzani wao katika dakika ya 30 baada ya mshambuliaji wao hatari kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa timu ya Mahakama ya Rufani, Spear Mbwembwe.
Kipindi cha pili kilianza
kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu. Timu ya Mahakama ya Rufani ilifanikiwa
kusawazisha bao dakika ya 20 ya mchezo na ku-‘level score board.’ Dakika chache
kabla ya mchezo kumalizika, winga hatari wa timu ya Mahakama Kuu aliukwamisha
wavuni mpira na kusababisha mechi hiyo kumalizika kwa timu yake kuibuka wababe.
Katika mchezo wa pete,
Mahakama Kuu pia iliwabugiza Mahakama ya Rufani vikapu 25 kwa 11 huku Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma akiibuka
kinara wa kutupia vikapu golini. Hii iliwashangaza wengi na kuibua shangwe kila
kona wakati alipokuwa anatupia tupia vikapu hivyo.
Mchezo wa ‘draft’ uliowakutanisha
wanaume kutoka Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, ulichezwa kwa ustadi mkubwa,
huku mashabiki wa pande zote mbili wakianikiza na kuhamasisha ili wawakilishi
waweze kupata ushindi. Hata hivyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Issa Maige alifanikiwa
kumtoa kijasho chembamba Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Isaya Arufani na kuibuka
mshindi.
Katika mchezo wa karata, timu ya Mahakama ya Rufani wanawake imeibabua Mahakama Kuu, huku upande wanaume timu ya Mahakama Kuu ikawabamiza Mahakama ya Rufani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni