Jumanne, 5 Septemba 2023

KITABU CHA MKUSANYIKO MASHAURI YA UNYANYASAJI KINGONO KWA MTOTO CHAZINDULIWA

Na Faustine Kapama-Mahakama na Sade Soka (UDSM).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 05 Septemba, 2023 amezindua kitabu cha mkusanyiko wa mashauri ya ukatili wa kingono kwa mtoto wa Ireland na Tanzania na kuhimiza wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoaji haki kuongeza matumizi ya vina saba (DNA) katika kukusanya ushahidi ili kuwatia hatiani au kuwaachia huru wanaohusishwa kutenda uhalifu dhidi ya watoto.

Mhe. Prof. Juma amesema kuwa kuna matumizi ya chini ya DNA katika makosa ya ngono na imekuwa nadra katika Mahakama ya Rufani kusikiliza rufaa ambapo DNA imetumika katika ukusanyaji wa ushahidi. “Tunashangaa kwa nini, huku sheria iko wazi kabisa kwa sababu DNA inaweza kuwatia hatiani na pia kuwaondolea hatia wasio na hatia.

"Je, siyo wakati na sisi pia kupata uzoefu kutoka Ireland jinsi ushahidi wa DNA unavyotumika? Kuna mengi ambayo tunaweza kujifunza kutokana na Kitabu hiki na lengo hapa liwe kubadili mtazamo wetu na hata kubadili namna ya kuzitazama sheria tulizo nazo na kuzipa mwelekeo tofauti,” amesema.

Jaji Mkuu amesema kuwa Tanzania inapaswa pia kujifunza mbinu bora ya kurekodi ushahidi wa mtoto kutoka Ireland, ambayo ina vifungu vya sheria vinavyoruhusu ukusanyaji wa ushahidi kwa njia hizo.

Amesema hatua hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa Tanzania, hasa pale ambapo ni jambo la kawaida kwa Mahakama kusikiliza ushahidi wa watoto wahanga miaka kadhaa baada ya kutendeka kosa na mtoto anaweza asiwe na kumbukumbu nzuri anapohojiwa mahakamani.

“Kwa hivyo, kurekodi ushahidi mapema iwezekanavyo wakati mwingine kunasaidia sana kupata haki. Haya ni mafunzo, ambayo nadhani tunapaswa katika maboresho yetu, tuhakikishe tunaiga sheria za Ireland,” Prof. Juma amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Margaret Gaynor alipongeza mtazamo unaochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhusu hatua za kupinga ukatili wa kijinsia, ikiwemo kutunga sheria na kuimarisha uwezo wa utoaji haki kwa makosa ya jinai.

Naibu Balozi alisema kuundwa kwa kamati ya kuchunguza utendaji wa taasisi za makosa ya jinai nchini ni hatua nzuri ambayo Serikali imeichukua na ripoti iliyotolewa imezingatiwa na wote wanaohusika.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la IJA, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alisema kuwa Kitabu hicho kitakuwa nyenzo muhimu siyo kwa maofisa wa Mahakama pekee, bali pia Mawakili, Waendesha Mashtaka, Wapelelezi, Watunga Sera, Wasomi na umma kwa ujumla.

Awali katika salamu zake za ukaribisho, Mkuu wa IJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alisema uzinduzi wa Kitabu hicho umewezekana kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya Chuo hicho na Irish Rule of Law International (IRLI), shirika lisilo la kiserikali.

"Tuliingia makubaliano ya ushirikiano katika maeneo kadhaa katika kushughulikia eneo zima la unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, ikiwemo kuandaa Mkusanyiko wa kesi za namna hiyo kwa Tanzania na Ireland kwa sababu sote tunapata matatizo yanayofanana," alisema.

Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na umeratibiwa na Chuo cha IJA kwa kushirikiana na IRLI kupitia ufadhili wa ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.

Hafla hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Majaji Wafawidhi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama Kuu divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Mirathi na Ndoa, Temeke, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, pamoja na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Wengine ni Msajili wa Mahakama Kuu, wawakilishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi Tanzania na Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha mkusanyiko wa mashauri ya ukatili wa kingono kwa mtoto wa Ireland na Tanzania. Uzunduzi huo umefanyika leo tarehe 05 Septemba, 2023 jijini Dar es Salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akisoma kitabu kimoja. Anayeshuhudia kushoto ni Naibu Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Margaret Gaynor.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akimkabidhi Naibu Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Margaret Gaynor kitabu hicho.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la IJA, Mhe. Dkt. Gerald Ndika (kushoto) akipokea kitabu hicho kutoka kwa Jaji Mkuu.
Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Bi. Victoria Mgonela (kushoto) akipokea kitabu hicho kutoka kwa Jaji Mkuu.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria uzinduzi huo.
 Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi mbalimbali.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama.
 Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na kamati ya maandalizi.
(Picha na Magreth Kinabo)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni