Jumanne, 5 Septemba 2023

MAFUNZO YANAYOTOLEWA NA 'IJA' YAWE CHACHU YA KUJIJENGEA UWEZO; JAJI DKT. MASABO

Na Eva  Leshange- Mahakama, Singida

Jaji Mfawidhi  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo amewaasa watumishi kutumia fursa ya mafunzo yananayotolewa na chuo cha Uongozi Lushoto (IJA) katika kujijengea uwezo wakati wanasubiri fursa za kwenda masomoni.

Mhe. Dkt. Masabo aliyasema hayo hivi karibuni katika ziara yake ya kikazi ya ukaguzi Mahakama ya Wilaya Manyoni.

“Nasisitiza kwa watumishi wote kujenga utamaduni wa kufuatilia mafunzo ya mtandaoni yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto-IJA ili kujijengea uwezo, kwani ulimwengu haujasimama tunayo mengi ya kujifunza”

Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Mhe. Dkt. Masabo aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi kwa kazi nzuri wanayofanya hasa katika usikilizwaji wa mashauri, na kwa mkakati waliouweka katika kuondokana na mashauri ya mlundikano (Backlog Stopping).

Aliongeza kuwa, kwa Mahakama za Mwanzo shauri linatakiwa kuisha ndani ya miezi mitatu (3) tangu kufunguliwa kwake na kwa upande w amashauri ya wilayani yanatakiwa kuisha ndani ya miezi 9 tangu kufunguliwa kwake.

Akipokea taarifa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni katika kipengele cha mirathi, amesisitiza malipo ya mirathi kufanyika ipasavyo kwa wanufaika na kwa upande wa mirathi ambazo bado hazijatambulika jitahada binafsi zifanyike kwa kufanya upekuzi kwa majalada yote ambayo bado hayajafungwa ili kubaini kama kuna wanufaika ambao bado hawajalipwa. 

Akizungumzia kuhusu nakala za hukumu amesisitiza zitolewe mara tu hukumu inapomalizwa kusoma na si vinginevyo.

Katika ziara yake Wilayani hapo alipata fursa ya kutembelea Gereza la Wilaya Manyoni na kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu. Aidha, aliwapongeza wadau wote wa haki jinai kwa kazi nzuri wanayofanya kwani hali ya gereza ilonekana ni nzuri hakuna msongamano na changamoto zote zilizoibuliwa zilitatuliwa.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo Manyoni wakisalimiana na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Dkt. Juliana Masabo alipowasili mahakamani hapo kwa ziara ya kikazi hivi karibuni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi  Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe  Alisile Mwankejela akisoma taarifa mbele ya  Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo (aliyeketi mbele katikati). Wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe.Sylvia Lushasi na  aliyeketi wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni  wakimsikiliza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo (hayupo pichani) aliyeketi katikati ni Bi. Geradina Machumu, Afisa Utumishi Mahakama ya Wilaya Manyoni.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo aliyeketi mbele (katikati) akizungumza na watumishi (hawapo pichani).



 Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo akisalimiana na wajumbe wa haki jinai alipowasiri Gereza la Wilaya Manyoni kwa ajili ya ukaguzi.


(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni