Jumatatu, 4 Septemba 2023

UGOMVI WA WAZAZI USIATHIRI WATOTO; MHE. LYIMO

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha Pwani, Mhe. Judith Lyimo amewataka wazazi wanapokuwa na ugomvi kutowajaza maneno mabaya watoto ya kumchukia mzazi mmojawapo bali wawapende wote ili kuondoa mgawanyiko.

Akitoa elimu kuhusu Sheria ya Mtoto katika ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo leo tarehe 04 Septemba, 2023, Mhe. Lyimo amesema endapo kuna utofauti au ubaya wa mzazi mmojawapo Watoto wataujua wenyewe pindi wakiweza kuchanganua pasipo kuambiwa na mzazi mmojawapo.

“Mara nyingi wazazi wanapogombana na kuwahusisha watoto inasababisha kuathirika kisaikolojia katika kutengana kwa wazazi mtoto anapaswa kujua familia zote mbili ya baba na ya mama,” amesema Mhe. Lyimo.

Ameongeza kwa kusisitiza wazazi kutowalisha sumu watoto kumchukia mzazi mmojawapo bali wawapende wote na utofauti au ubaya wa mzazi mmoja wataujua wao wenyewe pindi wakiweza kuchanganua mambo.

“Ni haki ya kila mzazi kukaa na mtoto wake ikitokea mmetalikiana basi kuna utaratibu wa kukaa na mtoto kwa kila mzazi anapewa siku zake lengo lake mtoto ajue pande zote mbili” ameeleza Mhe. Lyimo.

Akijibu swali na mwananchi mmojawapo aliyekuwa mahakamani hapo ( ambaye hakutaka jina lake lijulikane) alilouliza kwanini baba tu ndio ana wajibu wa kutoa pesa ya matunzo wakati mama nae ana uwezo? Mhe. Lyimo amesema Mahakama inaangalia uwezo wa pande zote mbili kabla ya kutoa uamuzi kwa hiyo uamuzi utatoa haki sawa kwa wote katika matunzo na pia mtoto anatakiwa kuchagua aishi na nani kati ya mama au baba halazimishwi kuishi kwa mama tu.

Kadhalika, amesema kwamba Mahakama inaangalia maslahi mapana ya mtoto kama vile mazingira anayoishi aliyeleta maombi ya kuishi na mtoto kama sio mazuri Mahakama itapata taarifa kutoka kwa Maafisa Ustawi wa Jamii na ndipo itatoa uamuzi.

Akijibu swali lingine la mwananchi huyo alilouliza kuhusu mtoto ambaye hana wazazi na anatakiwa kulipa faini hakuna mtu wa kumlipia Mahakama itafanya nini? Mhe. Lyimo amesema  mtoto akikamatwa lazima Ustawi wa Jamii wawepo na hata katika kuendesha kesi Ustawi wa Jamii wanapaswa kuhusika kwa mujibu wa Sheria.

Ameongeza kwamba, ikifika hatua ya hukumu Ustawi wa Jamii wataitaarifu Mahakama kuwa, mtuhumiwa ambaye ni mtoto hana wazazi na Mahakama inatoa adhabu ya kwenda Chuo cha Mafunzo ambapo kwa Tanzania kipo mkoani Mbeya. 

Akizungumzia kuhusu mashauri ya jinai yanayoweza kumkabili mtoto, Mhe. Lyimo amesema mtoto hata kama akikutwa na hatia katika makosa ya jinai wazazi wake watapaswa kulipa faini maana Sheria hairuhusu kumfunga mtoto. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Judith Lyimo akitoa elimu kuhusu  Sheria ya Mtoto  katika ukumbi wa Mahakama ya Wazi uliopo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani.

Baadhi wa wananchi waliofika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani wakifuatilia elimu iliyokuwa ikitolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Judith Lyimo (hayupo katika picha).

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni