Jumatatu, 4 Septemba 2023

JAJI MONGELA AWAKUMBUSHA MAJAJI, MAHAKIMU KUTUNZA TUNU YA UADILIFU.

Na. Paul Mushi- Mahakama, Moshi

Majaji na Mahakimu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, wametakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu, usawa na kuheshimu utawala wa Sheria katika kutekeleza jukumu lao la utoaji haki, ili kuendelea kukuza imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lilian Mongela wakati akifungua mafunzo ya Majaji na Mahakimu wa Kanda hiyo, yanayofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, yakiwa na lengo la kuwajengea uelewa wa umuhimu wa maadili kwa viongozi wa umma na kujikumbusha mambo ambayo wanapaswa kuepuka katika utendaji wao wa kazi.

Mhe. Dkt. Mongela amesema, maendeleo ya nchi yoyote duniani yanategemea kwa kiasi kikubwa uzingatiaji wa maadili katika kusimamia rasilimali za taifa na katika utoaji wa huduma bora katika sekta ya umma na binafsi na kwamba uongozi wa umma ndiyo chachu ya kuleta usawa, umoja, upendo, amani na kuheshimu utawala wa sheria.

"Uongozi wa umma ndiyo chachu ya kuleta usawa, umoja, upendo, Amani na mfano wa kuheshimu utawala wa sheria, na katika muhimili wetu,  sisi tukiwa watu tulioaminiwa kutoa haki kwa jamii suala hili ndilo linapaswa kuwa kipaumbele chetu cha kila siku ili kutokuondoa imani kwa wale wanaotutegemea kujipatia haki"amesema Mhe. Dkt. Mongela.

Ameongeza kuwa "Ni imani yangu kuwa, uelewa na ujuzi mtakaoupata kupitia mafunzo haya utaimarisha waledi mlio nao na kuhakikisha jukumu la msingi la Mahakama la utoaji haki linatekelezeka katika misingi ya uadilifu, na kukuza zaidi imani ya wananchi kwenye Mahakama zetu"

Jaji Mfawidhi huyo alisema, mafunzo hayo yatawasaidia kujikumbusha jukumu lenu la msingi la utoaji haki na kuongeza uelewa wa pamoja juu ya mambo gani ambayo mnapaswa kuyaepuka kama viongozi ili kulinda heshima ya muhimili wa Mahakama. Wakufunzi wameandaa mambo mazuri ambayo yatasaidia kwenda kufanya mabadiliko katika masuala yahusuyo maadili na hivyo kuwa kioo kwa wale mnaowahudumia katika nafasi zenu.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Omari Kingwele alisema, Mahakama ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mafunzo hayo yatasaidia kujiimarisha na kujisafisha ili kuondoa malalamiko ya wananchi ya mara kwa mara.

"Zikichambuliwa taasisi ambazo zinalalamikiwa na watu Mahakama haikosekani miongoni mwa taasisi 10 zinazotajwa na hii inatokana na kwamba tunahudumia kundi kubwa la watu na katika mfumo wetu wa maamuzi anayeshinda kashinda na anayeshindwa kashindwa, hivyo tunahitaji sisi wenyewe kwanza kujisafisha ili kule kunyooshewa kidole ibaki kwenye dhana na si uhalisia", aliongeza Naibu Msajili huyo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Bw. Donald Makawia alisema mafunzo hayo ni sehemu ya sera ya Mahakama ya kuwajenga watumishi uwezo na kuwakumbusha majukumu yao ikiwa sambamba na suala la maadili wawapo kazini hatua ambayo itawawezesha kuzingatia uadilifu na pindi wanapotekeleza majukumu yao.

"Majaji na Mahakimu, wao ndiyo watoa haki hivyo wanapaswa kuwa waadilifu, waaminifu katika kazi yao ya kutoa haki mahakamani na kuzingatia miiko na kanuni zote za maadili ya utumishi wa umma wanapofanya kazi zao za kila siku, kila mmoja atambue uzingatiaji wa maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa ni jukumu lao katika kuhakikisha wananchi wanapata haki", alisema Bw. Makawia

Hakimu Mkazi wa Mahakama Wilaya ya Rombo, Mhe. Atupele Mwanjala ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema yatawasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku kwani kazi hiyo inahitaji maadili kwa kiasi kikubwa ili kutoa haki kwa wananchi.

Mafunzo hayo ambayo yanatolewa na wakufunzi kutoka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) na Tume ya maadili, yamejikita kwenye mada mbalimbali ikiwemo Takukuru na majukumu yake, Mgongano wa Maslahi, baadhi ya makosa ya Rushwa yanayoonekana na kutendeka mahakamani, ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma pamoja na athari za kutozingatia maadili kazini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Dkt. Lilian Mongela (katikati walioketi) akiwa kwenye picha pamoja na washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mahakama za Wilaya na Mwanzo, yaliyofanyika hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Makazi mjini Moshi, wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Safina Simfukwe (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Adrian Kilimi (kulia).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Dkt. Lilian Mongela akifungu rasmi mafunzo hayo katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Safina Simfukwe (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Adrian Kilimi (kulia) wakifuatilia mada katika mafunzo hayo.


Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mahakama za Wilaya na Mwanzo walioshiriki mafunzo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Makazi mjini Moshi.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Omari kingwele (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi Bw. Donald makawia (kulia) wakifuatilia mafunzo hayo. 

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha- Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni