Jumatatu, 4 Septemba 2023

MAHAKAMA SIMIYU YAANZISHA CLAB YA SHERIA SHULE YA SEKONDARI BARIADI

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Katika kutekeleza nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/21– 2024/25), Mahakama Mkoa wa Simiyu imefanikiwa kuanzisha Club ya Sheria na kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi.

Mahakimu wanne pamoja na wanafunzi wa wanaosoma sheria kutoka vyuo mbalimbali hivi karibuni walitoa mada kadhaa kuhusu sheria kwa wanafunzi wapatao 300 kutoka Shule ya Sekondari Bariadi.

Timu hiyo ya kutoa elimu iliongozwa na Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Mary Nyangusi, ambaye aliwaeleza juu ya muundo wa Mahakama na Mpango Mkakati wa Mahakama, hasa katika kutekeleza nguzo ya tatu.

“Lengo kuu la kuanzisha Club za Sheria mashuleni ni kuwajengea uwezo wanafunzi waweze kutambua haki zao za msingi, waweze kuwa na uelewa mzuri juu ya sheria na kuwahamasisha kupenda kusoma sheria. Tumelazimika kuja na wanafunzi wanaosoma sheria kwa vitendo kutoka vyuo mbalimbali ili muweze kuhamasika zaidi,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Bw. Godfrey Masunga alifurahi kuanzishwa kwa Club ya Sheria shuleni kwake, kwani ndio ilikua kiu kubwa kwa wanafunzi wake. “Nimefurahi sana kwa ujio wenu, kwani vijana wangu watajifunza mambo mengi kuhusu sheria na haki zao kiujumla,” alisema Bw. Masunga.

Wanafunzi kutoka shule hiyo, baada ya kupata elimu hiyo waliuliza maswali mbalimbali, ikiwemo kutaka kujua kwa nini mshtakiwa akiachiwa huru ndani ya mwezi mmoja haruhusiwi kupiga kura na njia zinazotumika kumkamata mtu anayedaiwa kufanya mauaji na kukimbia je ya nchi.

Pia wanafunzi walitaka kujua vitu gani kwenye Katiba ya Tanzania vinahitaji kufanyiwa marekebisho, kwanini sheria isianze kufundishwa kuanzia elimu ya chin. Maswali hayo yalijibiwa kwa usahihi na timu nzima iliohudhuria kikao hicho cha uzinduzi wa Club ya Sheria.

Naye Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, akifunga mkutano huo aliwaomba wanafunzi na walezi wa Club hiyo kutembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Bariadi ili kujionea namna Mahakama hizo zinavyofanya kazi.


Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Mary Nyangusi akitoa elimu juu ya sheria kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi mkoani Simiyu.

Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Bariadi wakiwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi pamoja na mwanafunzi anayejifunza kwa vitendo katika Mahakama ya Mwanzo Somanda.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi wakisikiliza kwa makini elimu inayotolewa na timu ya Mahakama juu ya sheria.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Bw. Godfrey Masunga akiwakaribisha watumishi wa Mahakama waliokuja kutoa elimu na kuanzisha Club ya Sheria shuleni hapo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni