Na Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) imeingia kambini rasmi kujiwinda na mashindano ya
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia
kuanza mwishoni wa mwezi huu wa Septemba, 2023 mkoani Iringa.
Akizungumza katika
viwanja vya mazoezi vilivyoko Shule ya Sheria maeneo ya Mawasilisho jijini Dar
es Salaam, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewahimiza wanamichezo
wote kufanya mazoezi kwa kujituma na kuzingatia programu ya mwalimu ili
kumwezesha kuunda kikosi imara kitakachoiwakilisha vyema Mahakama ya Tanzania
kwenye mashindano hayo.
"Tumeingia rasmi
kambini, wachezaji wote tuliowaita kutoka Mikoa yote wameshawasili na tayari
wameshaanza mazoezi katika michezo mbalimbali tunayotarajia kushiriki kwenye
mashindano. Niwakumbushe wanamichezo wenzangu kuwa mashindano ya SHIMIWI siyo
lelemama," alisema.
Dede amemtaka kila
mwanamichezo kuonyesha bidii na umakini kwenye mazoezi ili aweze kuchaguliwa
kwenye timu itakayoundwa na kupeperusha bendera ya Mahakama kwenye mashindano hayo
kwani anaamini watakuwa na timu imara ambayo itashangaza wengi.
"Mwaka huu tuna
vijana wazuri sana kwenye kila mchezo. Kinachotakiwa ni wao kumshawishi mwalimu
ili awaingize kwenye kikosi chake. Tunao wataalamu ambao wanamfuatilia kila mmoja
namna anavyojitoa kuitumikia Mahakama na kuonyesha nidhamu. Niwaombe wenzagu
wakubali kujitoa na kuonyesha uzalendo kwa Mahakama ili tuweze kupata ushindi
kwenye michezo yote,” amesema.
Ameonya wapinzani wao kuwa
safari hii wataambulia makalayi kwani wamejipanga kuzoa kila kitu kwenye
mashindano hayo. "Hatutakuwa na utani na mtu safari hii, waanze kujiandaa
kisaikolojia na hatutakubali hujuma ya aina yoyote. Ingawa tutapiga pale pale
kwenye mshono, tunawaomba wenzetu wavumilie kitakachowakuta,"alionya.
Michezo ambayo Mahakama
Sports inatarajia kushiriki katika mashindano hayo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake,
Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake
pamoja na Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni