·Yaikandamiza Ras Kilimanjaro vikapu 49
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Netiboli imeyaanza vyema mashindano ya
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) leo tarehe 29
Septemba, 2023 baada ya kuiadhibu vikali timu ya Ras Kilimanjaro kwa jumla ya
vikapu 49:6.
Katika mchezo huo
uliochezwa majira ya alasili, timu ya Mahakama ilienda mapumziko ikiwa
imeshatumbukiza vikapu 31kwa 2 na kuifanya kuongeza katika kipindi cha
kwanza.
Baada ya mapumziko,
Mahakama Sports waliendelea kulisakama lango la Ras Kilimanjaro na waliwabana
pumzi wapinzani wao wasifurutike hadi dakika ya mwisho.
Tupia tupia ya vikapu
iliendelea, huku timu ya Mahakama ikiwachachafya wapinzani wao. Hadi mwamuzi
anapuliza kipenga cha mwisho, Mahakama Sports ilikuwa imeshatupia vikapu 49 kwa
6 walizoambulia wapinzani wao, Ras Kilimanjaro.
Akizungumza baada ya
mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema kipigo hicho
kitaendelea na ni onyo kali kwa yule atakayethubutu kuwachezea.
"Nilisema tangu
mwanzo, hatutamchekea mtu tusije tukaambulia mabua. Sisi tunachotaka ni
makombe. Natoa onyo, wasijaribu kutuchezea, wataumia," Mwenyekiti Dede
ameonya.
Naye Mwalimu wa Timu Paul
Mathias amewapongeza vijana wake kwa kuonyesha mchezo mzuri na kuzingatia
maelekezo aliyowapa. "Kama tutaendelea hivi, kuna mtu atakula mia hapa.
Hatuna utani na mtu sisi," amesema.
Wachezaji walioiwakilisha Mahakama ni Tatu Mawazo, Philomena Haule, Upendo Gustav, Nyangi Kisangenta, Shani Ally, Eunice Chengo na Sophia Songoro. Waliokuwa kwenye mbao ndefu ni Leah Danda, Agnes Mwanyika, Lulu Nchimbi, Rohiba Makassi, Malkia Nondo, Angela Dismas, Akinzia Kimaro na Lucy Kibona.
Matokeo hayo ni
mwendelezo wa ushindi ambao timu za Mahakama zimeupata. Mapema leo asubuhi,
Mahakama Sports Kamba Wanaume na Kamba Wanawake walianza vizuri mashindano hayo
baada ya kutembeza vipigo kwa wapinzani wao Ras Kigoma na Waziri Mkuu Sera
ambao waliamua kuingia mitini.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, Mahakama Sports inatarajia
kuvaana na timu zingine 14 ili kupata nafasi ya kutinga 16 bora.
Katika mpira wa miguu,
timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji,
RAS Kigoma na Kilimo, timu ya netiboli ya Mahakama imepangwa katika kundi G na
itapepetana na timu za Ardhi, RAS Kilimanjaro na Elimu.
Kwenye mchezo wa Kamba Wanaume,
timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itaumana na TAKUKURU, RAS Kigoma,
Mawasiliano na Ardhi na Kamba Wanawake imepangwa kundi A pia na itakabiliana
vilivyo na timu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya
Uchaguzi (NEC).
Mahakama Sports inashiriki
katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira
wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hawa hapa vijana wa Professa walioipeperusha vyema bendera ya Mahakama.
Hatimaye mpira ukajaa kwenye nyavu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni