Ijumaa, 29 Septemba 2023

WANANCHI MKOANI KATAVI WAIPONGEZA MAHAKAMA UTOAJI ELIMU YA SHERIA

-Waomba zoezi liwe endelevu

Na James Kapele – Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi

Wananchi mkoani Katavi wameipongeza Mahakama ya Tanzania mkoani humo kwa kuisimamia ipasavyo programu ya utoaji wa elimu ya Sheria inayotolewa kabla ya muda wa kuanza kwa mashauri mahakamani kwa wananchi wanaohudhuria katika Mahakama hiyo . 

Wametoa pongezi hizo leo tarehe 29 Septemba, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye alipokuwa akitoa elimu katika ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo. 

“Mheshimiwa, binafsi naomba kuipongeza Mahakama yote kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa kuanzisha jambo hili ambalo kwa hakika limetusaidia sana kutuongezea uelewa katika masuala mbalimbali ya kisheria ambayo hatukuwahi kuyafahamu kabla,” amesema Mzee Kendson Mbugi mmoja kati ya wananchi waliokuwepo mahakamani hapo.

Mzee Mbugi ameiomba Mahakama jambo hili liwe endelevu kwa kuwa litawasaidia kupunguza migogoro katika jamii.

Mara baada ya Mhe. Sumaye kuhitimisha zoezi la kutoa elimu, baadhi ya wananchi wamesema Mahakama imefanya jambo kubwa na la kuigwa ambalo limekuwa likiwasidia kujifunza mambo mbalimbali ya sheria na hivyo kuishukuru kwa kuona umuhimu wa kuanzisha jambo hilo.

Mahakama mkoani Katavi imejiwekea utaratibu wa utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi wanaofika mahakamani hapo, elimu hutolewa kabla ya kuanza kusikilizwa kwa mashauri. Hili ni moja kati ya malengo mahsusi ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Mzee Kendson Mbugi (aliyesimama) Mkazi wa Kijiji cha Katsunga mkoani Katavi akitoa pongezi na neno la shukrani kwa Mahakama mara baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye kutoa elimu ya sheria leo tarehe 29 Septemba, 2023. Wengine ni sehemu ya wananchi waliopata elimu iliyokuwa ikitolewa na Hakimu huyo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria programu hiyo (hawapo katika picha).

 Sehemu ya wananchi waliokuwepo mahakamani hapo wakifuatilia wakimsikiliza Mhe. Sumaye (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa elimu.

Aliyesimama ni moja kati ya wananchi akiuliza swali wakati wa majadiliano.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni