Ijumaa, 29 Septemba 2023

MAHAKAMA SPORTS YAANZA MAMBO YAKE

·Kamba Wanaume yawang'oa pua Ras Kigoma

·Kamba Wanawake wakimbiwa

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa

Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika mkoani hapa yameanza leo tarehe 29 Septemba, 2023, huku timu ya Mahakama (Mahakama Sports) ikiibuka mshindi kwenye michezo yote miwili ya kamba.

Kamba Wanaume imenyonyoana na timu ya Ras Kigoma, huku timu ya Wanawake ikizoa pointi zote mbili baada ya Waziri Mkuu Kazi kuingia mitini ili kukwepa kichapo cha mwizi wa mayai.

Ilikuwa timu ya Kamba Wanawake iliyoanza kuitwa uwanjani majira ya saa 12.45 asubuhi. Kabla ya mchezo kuanza, waamuzi waliamua kuusimamisha ili kuisubiri timu kutoka Waziri Mkuu Kazi. Baada ya kuita kwa mara kadhaa, timu ya Mahakama ikaamuriwa icheze peke yake na kuzoa pointi zote mbili.

Baada ya kukamilika kwa mchezo huo, timu za Kamba Wanaume ziliingia uwanjani, huku Mahakama Sports ikipangwa na Ras Kigoma. Baada ya mchezo kuanza, Mahakama Sports haikuwa na huruma na mtu, iliwakamua kisawasawa timu pinzani katika awamu ya kwanza. 

Awamu ya pili ilipoanza, Ras Kigoma walijaribu kuwaragai waamuzi kwa kuvuta kamba kabla ya filimbi kupigwa. Hata hivyo, waamuzi walishtukia janja janja hiyo na kurejesha kamba kwenye mstari.

Baada ya mwamuzi kupuliza kipenga kuashiria kuanza kwa mchezo, timu ya Mahakama ilikuwa kama Nyati aliyejeruhiwa na kuwaburuza vibaya Ras Kigoma, hivyo kuondoka na pointi zote mbili.

Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza vijana wake kwa kuonyesha mchezo mzuri na kupata ushindi huo mkubwa. Amesema kuwa huo ni mwanzo mzuri katika mashindano hayo.

"Nawapongeza wachezaji wote kwa ushindi huu ambao unaonyesha nia yetu iliyotuleta kwenye mashindano haya. Tutaendelea kupambana kwenye michezo ijayo na safari hii hakuna atakayechomoka salama, labda watukimbie," amesema.

Baadaye majira ya mchana kutakuwepo na mechi nyingine ambapo timu ya Mahakama ya Netiboli ambayo ipo kundi G inatarajia kupepetana na Ras Kilimanjaro. 

Mchezo wa mpira wa miguu wa kundi A kati ya Mahakama Sports na Kilimo uliokuwa uchezwe leo majira ya asubuhi umeahirishwa hadi siku nyingine kufuatia Kilimo kufiwa ghafla na Nyanda wao tegemezi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa kuhusu mashindano haya, Mahakama Sports inatarajia kuvaana na timu zingine 14 ili kupata nafasi ya kutinga 16 bora.

Katika mpira wa miguu, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo, timu ya netiboli ya Mahakama imepangwa katika kundi G na itapepetana na timu za Ardhi, RAS Kilimanjaro na Elimu.

Kwenye mchezo wa Kamba Wanaume, timu ya Mahakama imepangwa kundi A na itaumana na TAKUKURU, RAS Kigoma, Mawasiliano na Ardhi na Kamba Wanawake imepangwa kundi A pia na itakabiliana vilivyo na timu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Mahakama Sports inashiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Timu ya Mahakama ya Kamba Wanaume (juu) ikitoa kichapo kwa timu ya RAS Kigoma(chini).

Timu ya Mahakama ya Kamba Wanawake kwa raha zao baada ya Waziri Mkuu Kazi kula kona.
Timu ya Mahakama ya Kamba Wanaume tayari kwa mchezo.
Timu ya Mahakama ya Kamba Wanawake wapo tayari kwa kazi.
Miamba hiyo hapo, kuna mtu atanyolewa kwa chupa safari hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni