· Mahakama Sports kumenyana na timu 14 kuwania 16 bora
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Ratiba ya makundi katika
mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
yanayoanza kufanyika mkoani hapa imeshawekwa hadharani, huku Timu ya Mahakama
ya Tanzania (Mahakama Sports) ikitarajia kuvaana na timu zingine 14 ili kupata
nafasi ya kutinga 16 bora.
Katibu wa Mahakama Sports
Robert Tende amesema kuwa katika mpira wa miguu, timu ya Mahakama imepangwa
kundi A na itachuana na Viwanda na Biashara, Maji, RAS Kigoma na Kilimo.
Ameeleza pia kuwa timu ya
netiboli ya Mahakama imepangwa katika kund G na itapepetana na timu za Ardhi, RAS
Kilimanjaro na Elimu, huku kamba wanaume ikipangwa kundi A na itaumana na TAKUKURU,
RAS Kigoma, Mawasiliano na Ardhi.
Timu ya kamba wanaume ya
Mahakama imepangwa kundi A pia na itakabiliana vilivyo na timu kutoka Tume ya
Utumishi wa Umma, Waziri Mkuu Kazi na Tume ya Uchaguzi (NEC).
Leo jioni tarehe 28
Septemba, 2023, Mahakama Sports imefanya mazoezi mepesi ili kujiandaa na
mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kesho tarehe 29 Septemba, 2023.
Mahakama Sports inayoshiriki
katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira
wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli iliwasili
mkoani hapa jana tarehe 27 Septemba, 2023 na kuzua gumzo kwenye viunga na mitaa
mbalimbali ya mji.
Mwenyekiti wa Mahakama
Sports Wilson Dede amesema vijana wote wapo salama na wapo tayari muda wowote
kushiriki katika mashindano na ameahidi kuibuka na ushindi kwenye kila mchezo
kutokana na ubora wa timu waliyonayo.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni