·Yazua gumzo kila kona
·Wenyewe watamba kutembeza vichapo mwanzo mwisho
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Iringa
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) imewasili mkoani hapa leo tarehe 27 Septemba, 2023
kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayotarajia kuanza kesho kutwa tarehe 29 Septemba, 2023.
Kuwasili kwa Timu hiyo
inayoshiriki katika michezo mbalimbali mwaka huu, ikiwemo Kamba Wanaume na
Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha na Baiskeli
kumezua gumzo kwenye viunga na mitaa mjini hapa na kufanya baadhi ya maeneo
kuzizima.
Kwenye baadhi ya mitaa
kulionekana watu wakiwa kwenye vikundi wakijadili ushindani utakavyokuwa wakati
wa mashindano na haikujulikana kama watu hao walikuwa wanatoka kwenye timu
pinzani au ni wakazi wa mjini hapa.
"Zile bendera zilizotandazwa
mbele ya mabasi kama za Mahakama vile. Sijui itakuwaje mwaka huu, maana
jamaa wapo vizuri sana hawa kwenye kila mchezo, hasa Kamba. Hawa ndiyo
baba lao, wengine ni mchekea tu," alisikika jamaa mmoja ambaye
hakufahamika jina lake akisema.
Akizungumza muda mchache
baada ya kufika Iringa, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema
wanamshukuru Mungu kwa kufika salama na wanamichezo wote wapo salama na wapo
tayari kwa mashindano.
"Wachezaji wote wapo
vizuri na tupo tayari kwa michezo ambayo ipo mbele yetu. Tumekuja kuendeleza
pale tulipoishia mwaka jana, safari hii kama hakutakuwa na figisu figisu
tutafanya maajabu,” alisema.
Naye Mwalimu wa Timu Spear
Mbwembe amebainisha kuwa mara baada ya kuwasili wachezaji wote wataenda moja
kwa moja kambini kujiwinda na mashindano yanayoanza tarehe 29 Septemba, 2023.
"Hatuna muda wa kupoteza, tuna kazi moja tu iliyotuleta, ni ushindi,"
amesema.
Katika mashindano ya
SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni