Jumatano, 27 Septemba 2023

NAIBU MSAJILI DAR ES SALAAM AWAKUMBUSHA MAHAKIMU PWANI KUTOA NAKALA ZA HUKUMU KWA WAKATI

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo amewataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo mkoani Pwani kutoa nakala za hukumu kwa wakati ili kuepuka kuwachelewesha wafungwa waliopo gerezani kukata rufaa. 

Akiwa katika ziara ya kikazi katika Gereza la Mkuza lililopo Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani aliyofanya jana tarehe 26 Septemba, 2023, Mhe. Sundi alizungumza na wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo ambapo alipokea changamoto zao mbalimbali ikiwemo kuchelewa kupata nakala za hukumu hivyo kukata tamaa ya kukata rufaa Mahakama ya Wilaya.

Akijibu hoja hizo, Mhe. Fimbo aliwakumbusha Mahakimu kutekeleza hilo sambamba na kuwakumbusha wafungwa hao juu ya haki yao ya kukata rufaa ambapo alisema “mnazo nafasi tatu za kukata rufaa hivyo msiridhike na adhabu za Mahakama za Mwanzo kateni rufaa Mahakama za Wilaya ili mjue hatima zenu.”

Akiendelea kupokea changamoto mbalimbali, Mhe. Fimbo na msafara wake walishangazwa na kitendo cha mfungwa aliyemaliza muda wake raia ya Ethiopia kumuomba Msajili huyo kuilazimisha Serikali ya Ethiopia kuwarejesha nchini  kwao wafungwa waliomaliza muda wao ambao wapo gerezani kwa kukosa nauli ya kurudi nchini kwao.

Baada ya kupokea lalamiko hilo, Mhe. Fimbo alimtaka Afisa Uhamiaji aliyekuwepo kwenye msafara wake kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo. 

Akieleza kwa kina kuhusu suala hilo, Afisa Uhamiaji aliyeambatana na msafara huo, Bw. Fadhili Festo alisema jitihadi zimefanyika za kuzungumza na Ubalozi wa Ethiopia nchini ambapo alisema wamewahi kumpeleka Balozi wa Ethiopia gerezani hapo ambaye alizungumza na wafungwa hao na mpaka sasa wameondoka wahamiaji 107 na waliobaki ni 26 tu kati ya Waethiopia 133 waliokuwepo katika Gereza hilo. Hivyo amewaomba wawe wavumilivu wakati ubalozi wao unashughulikia suala lao.

Awali akimkaribisha Naibu Msajili na msafara wake, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mkuza, Bw. Ibrahim Nyamka amesema Gereza hilo lina uwezo wa kuhifadhi waharifu 70, lakini mpaka jana tarehe 26 Septemba, 2023 lilikuwa na jumla ya ya waharifu 157 idadi inayoonyesha kuna msongamano katika Gereza hilo. 

“Kumekuwa na wimbi kubwa la wahamiaji haramu wanaomaliza vifungo vyao na kuendelea kukaa gerezani kusubiri taratibu za kurudishwa nchini kwao hivyo kuongeza msongamano gerezani,” alisema Bw. Nyamka.

Baada ya kuzungumza na wafungwa na mahabusu wa gereza hilo, Mhe. Sundi aliendelea na ziara yake kuelekea Mahakama ya Mwanzo Mlandizi ambapo alizungumza na watumishi wa Mahakama hiyo na kuwasisistiza kuwa, wanapaswa kuujua Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka (2020/2021-2024/2025) ambao kwa sasa umebakiza miaka miwili kukamilika.

Aidha, alimtaka Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Mlandizi, Mhe. Nabwike Mbaba kutenga muda wake kuwafundisha kifungu baada ya kifungu ili kujua nguzo zote tatu za Mpango huo.

Akizungumza katika kikao hicho, naye Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka alisisitiza utoaji wa nakala za hukumu kwa wakati pindi tu wanapomaliza kusoma hukumu ili kutekeleza waraka wa Jaji Mkuu wa kutoa nakala hizo mara tu Hakimu anapomaliza kusoma.

Ziara hii ya Naibu Msajili ni ukaguzi wa robo tatu ya mwaka, katika ziara yake aliambatana na Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi  Pwani, Bw. Moses Minga, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Judith Lyimo na Wadau wa Haki Jinai.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,  Mhe. Sundi Fimbo akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Mlandizi Kibaha-Pwani jana tarehe 26 Septemba alipofanya ziara katika Mahakama hiyo.

Picha ya pamoja na Wadau wa Haki Jinai Mkoa wa Pwani. Katikati ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo,   kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi, wa pili kulia ni Mkuu wa Gereza la Mahabusu la Mkuza, Bw. Ibrahimu Nyamka.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni