Jumanne, 26 Septemba 2023

JAJI MANGO AACHA ALAMA KITUO CHA USULUHISHI

Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma tarehe 26 Septemba, 2023 aliwaongoza watumishi kumuaga Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mango aliyekuwa kihudumu kwenye Kituo hicho baada ya kuhamishiwa katika Kanda ya Tabora.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho, Mhe. Maruma amemshukuru Jaji Mango kwa kazi nzuri iliyotukuka aliyoifanya kwa kipindi cha miezi 16 kabla ya uhamisho huo.

“Toka amekuja kwenye Kituo hiki, Mhe. Mango ameweza kushughulikia mashauri 164. Mashauri ya usuluhishi siyo mchezo, huu ni mchango mkubwa sana, kwa sisi tunaofanya usuluhishi tunaelewa, hii ni hatua kubwa sana,” alisema.

Jaji Mfawidhi amemwomba Mhe. Dkt. Mango kueneza ujuzi wa usuluhishi alioupata kwenye Kanda mpya anayoenda kuhudumu ili dhana hiyo iweze kusambaa katika Mahakama zote, kwani matunda yake yanaoneka.

Alisema kuwa taarifa ya uhamisho wa Jaji Mango ilimshtua kutokana na jinsi walivyokuwa wamejiwekea malengo ya pamoja katika kuwahudumia wadaawa na kuweka maazimio ya kiutendaji.

"Ukitolewa mguu wako mmoja halafu unaanza kutembea kwa kutumia mmoja lazima uanze kuwa na akili ya ziada ili lengo ulilojiwekea liweze kutimia. Hivyo, tunatakiwa kujifunza kitu, tukubali mabadiliko kwa sababu yanamaana sana," alisema.

Mhe. Maruma alieleza kuwa katika kipindi walichokuwa pamoja na Jaji Mango wamefanya maboresho makubwa katika utendaji na uongozi, ikiwemo kupata Mtendaji, Mhasibu na watumishi wengine.

Hivyo alimshukuru Mhe. Dkt. Mango kwa utumishi wake, huku akiamini kule anakokwenda atapeleka ujumbe mzuri kuhusu umuhimu na faida za usuluhishi katika kushughulikia mashauri ya madai.

"Usuluhishi ni hatua kama hatua zingine, huyu (Mhe. Dkt. Mango) anaenda kuwa balozi mzuri, anakwenda kuwa Mwalimu, siyo katika ngazi ya Mahakama Kuu tu bali pia katika Kanda nzima ya Tabora," alisema.

Jaji Mfawidhi alisema kuwa kwake yeye anajisikia fahari kwa utumishi wa Mhe. Dkt. Mango kwa vile anajua kule anakokwenda atafanya kazi kubwa na muhimu. Amesema kama Jaji  Mango atawafundisha Mahakimu wote wa Mahakama za Mwanzo kujua usuluhishi watasuluhisha kesi zote, fursa ambayo kwa Dar es Salaam hawakuipata.

Naye Mhe. Dkt. Mango aliwashuku wote kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa akihudumu katika Kituo hicho na kuahidi kuendeleza yote mema aliyojifunza kutoka kwao.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake, Mwangalizi wa Ofisi Bi Christina Nchimbi alimshukuru Jaji Mango kwa upendo na ushirikiano mkubwa aliouonesha kwa kipindi chote cha miezi 16 alipokuwa akihudumu katika Kituo hicho.

Alimtakia kila la heri kwenye kituo chake kipya na kumwomba Mungu amzidishie neema na baraka katika utumishi wake.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma akifafanua jambo alipokuwa anaongea na watumishi wa Kituo hicho katika hafla fupi ya kumuaga Jaji Dkt. Zainab Mango (hayupo kwenye picha).
Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma (kushoto) akigongesha 'glass' na  Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Zainab Mango katika  hafla hiyo.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika Kituo cha Usuluhishi (juu na chini) wakiunga na Jaji Mfawidhi, Mhe. Zahara Maluma kumtakia heri  Jaji Dkt. Zainab Mango kule anakokwenda.

Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma (kushoto) na  Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Zainab Mango wakikata keki. Picha chini, Mhe. Maluma akimrisha keki hiyo.


Mwangalizi wa Ofisi Bi Christina Nchimbi akiwasilisha salamu za shukrani kwa Jaji Zainab Mango kwa niaba ya watumishi wenzake.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama katika Kituo cha Usuluhisi (juu na chini) waliohudhuria hafla hiyo. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni