Ijumaa, 20 Oktoba 2023

JAJI RWIZILE ASISITIZA MATUMIZI MAZURI YA RASILIMALI FEDHA

  • Ahimiza kuweka vipaumbele katika utekelezaji majukumu
Na Aidan Robert

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile  amewataka watumishi wa Kanda hiyo kutumia rasilimali fedha zinazopatikana kwenye vipaumbele pamoja na kuhakikisha kuwa, shughuli zinafanyika kwa ufanisi.

Akizungumza katika kikao na Viongozi wa Kanda hiyo kilichofanyika tarehe 19 Oktoba, 2023, Mhe. Rwizile alisema rasilimali fedha ndogo zinazopatikana zitumike kwenye vipaumbele vya Mahakama maaana bila kuwa na vipaumbele hawataweza kwenda kwa kasi inayotakiwa katika viwango vya Mahakama ya sasa.

Aidha, Jaji Rwizile aliwataka pia watumishi kutoa taarifa za utendaji wa kila wilaya na kuweka bayana changamoto zinazowakabili katika utendaji wao ili baadhi ya changamoto zinazoweza kukwamisha mpango mkakati wa Mahakama katika utendaji kazi.

Ameendelea kusisitiza kuhusu matumizi ya TEHAMA hususani katika kipindi hiki ambapo Mahakama ya Tanzania inahamia kwenye mfumo mpya wa kuendesha mashauri kwa njia kielekitroniki (Advance Case Management) na kusisitiza kuwa, Mahakama zote Kigoma zinapaswa kuimarisha miundombinu ya umeme na TEHAMA ili kuhakikisha majengo yote yana kuwa na miundombinu ya uhakika ili kutokwamisha usikilizwaji wa mashauri kwa kila Mahakama zetu hapa Kigoma.

Kadhalika, amewataka pia Viongozi na Maafisa katika Kanda hiyokufanya ukaguzi wa kila robo ya mwaka ili kutathmini utendaji wa shughuli zao ili kuboresha sehemu inayoonekana kulegalega au kukwama katika shughuli zao.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, alisema Kanda hiyo imejitaidi kutembea na Mpango Mkakati wa Mahakama katika nguzo zote tatu na kuongeza kuwa wamehakikisha kila mtumishi anaelewa Mpango huo.

"Kuhusu ujio wa mfumo mpya wa (e-Case Management) ambao utatumika hivi karibuni tumejipanga kuupokea na kufanyia kazi ikiwa ni kuimarisha miundombinu itakayo saidia utumiaji wa mfumo huo kwenye mahakama zetu, mpaka sasa wapo watumishi wanaendelea kuufanyia mazoezi ili kubaini baadhi ya changamoto ili kuziwasilisha kwenye mamlaka husika kwaajili ya kuzifanyia kazi," alisema Mhe. Mariki.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Benjamin Mlimbila, alisema Ofisi yake inaendelea kusimamia vema shughuli za Mahakama katika Kanda hiyo.

Kikao hicho kilichofanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Uvinza kilihudhuriwa na  wajumbe wote wa kamati ya uongozi ambayo inawajumuisha, Naibu Msajili, Mtendaji, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama zote za Wilaya, Maafisa Utumishi na Tawala, vilevile Wakuu wote wa Vitengo. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, akisaini kitabu cha wageni alipokuwa katika Ofisi Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Uvinza kwa ajili ya kikao cha pamoja na Viongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma.
Picha ya jengo la Mahakama ya Wilaya Uvinza ambapo kikao cha uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilipofanyikia.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) pamoja na Viongozi wenzake wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikijiri katika kikao. Kushoto ni  Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na kulia Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Benjamin Mlimbila. 
Wajumbe wa kikao wakifuatilia kwa makini maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Mhe. Rwizile, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Mwakitalu, Hakimu  Mkazi Mfiwidhi wailaya Buhigwe, akifuatiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mhe. Kyamba.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni