Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Kufuatia maboresho katika
upande wa matumizi ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayofanywa
na Mahakama ya Tanzania, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro
imefanikiwa kufunga vifaa vya kisasa vya mtandao kwenye Magereza ya Kilosa na Mahenge.
Vifaa hivyo vilifungwa na
Kaimu Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Tofiki Sumbuo
ili kurahisisha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (Video Conference)
kupitia mfumo wa Mahakama wa http://virtualcourt.judiciary.go.tz.
Akipokea vifaa hivyo, Mkuu
wa Gereza la Kilosa Deodatus Kazinga aliushukuru uongozi wa Mahakama ya
Tanzania kwa kuwarahisishia utoaji huduma na kuwapunguzia gharama za
kumsafirisha Mahabusu toka Magereza hadi mahakamani.
“Tunashukuru kwa Mahakama
ya Tanzania, hakika wameturahisishia shughuli ya utoaji huduma, wakati mwingine
tulikuwa tunapitia katika mazingira magumu ya kumsafirisha Mahabusu, hususani
katika mashauri ya ugaidi kutoka hapa Magereza kwenda mahakamani umbali wa kilomita
saba,” alieleza.
Naye Afisa TEHAMA wa
Kanda Said Tamimu alisema kwa upande wa Mahakama Morogoro tayari wamefanikiwa
kufunga vifaa vya kusikilizia mashauri kwa njia ya mtandao katika Magereza
manne ya Kibelege huko Ifakara, Gereza la Mahabusu lililoko Morogoro Mjini,
Gereza la Kilosa na Gereza la Mahenge.
Alisema kuwa kufungwa kwa vifaa hivyo kutarahisisha usikilizaji wa mashauri, ikiwemo kuondoa hatari inayoweza kujitokeza wakati wa kumsafirisha mahabusu toka gerezani hadi mahakamani, mfano kwenye mashauri yanayohusisha mashtaka ya ugaidi.
Mkuu wa Gereza la Kilosa Deodatus
Kazinja (kulia) akipokea kutoka kwa Kaimu Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Morogoro Bw. Tofiki Sumbuo nyaraka za makabidhiano ya vifaa
vya mtandao kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri.
Majaribio ya matumizi ya
Video Conference kutoka katika Gereza la Kilosa baada ya vifaa hivyo kufungwa.
Kaimu Afisa TEHAMA kutoka
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Tofiki Sumbuo (kulia)
akikabidhi vifaa vya Video Conference kwa Askari wa Gereza la Mahenge.
Vifaa vya Video
Conference vilipowasili katika Gereza la Kilosa na kupokelewa na Mkuu wa Gereza
Deodatus Kazinja (kushoto). Kulia ni Kaimu Afisa TEHAMA kutoka Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Tofiki Sumbuo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni