Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa
Chama cha Watendaji Wakuu wa Mahakama wa nchi zilizopo Kusini na Mashariki mwa
Afrika, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Tanzania ni moja kati ya nchi za
ukanda huo ambazo zimeonekana kuwa na sheria
bora ya Uongozi wa Mahakama.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo tarehe 19 Oktoba,
2023 jijini Arusha kuhusu Mkutano wa Watendaji Wakuu wa
Mahakama wa nchi zilizopo Kusini na Mashariki mwa Afrika, Mwenyekiti huyo amesema
Sheria Namba 4 ya Usimamizi wa Mahakama ya mwaka 2011 imewagusa wanachama wa
chama hicho kwa kuwa imetenganisha majukumu kati ya watumishi ambao ni Maafisa Mahakama
na wale wasiokuwa Maafisa Mahakama.
“Moja
ya mambo tutakayoyagusia kwenye mkutano wetu ni kuona hata namna ya kuitumia
sheria hiyo katika kupanua wigo wa utendaji kazi ili nchi nyingine ziweze
kujifunza sheria hii na kuona jinsi ya kuifanyia maaboresho’, alisema.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama amesema, Tanzania imeonekana kuwa kinara wa kuweza kuunganisha
Maafisa Mahakama na wasio Maafisa Mahakama wakati kwenye baadhi ya nchi kuna
mgongano kati ya watumishi hao wa Mahakama.
Akifafanua,
Prof. Ole Gabriel alisema Tanzania kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mahakama namba
4 ya mwaka 2011 imebainisha wazi majukumu ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili
Mkuu wa Mahakama na pia imetoa fursa ya kuwa na Watendaji kwenye kila Kanda hatua
inayosaidia kazi kufanyika kwa ufanisi.
Alisema
Mkutano wa Watendaji Wakuu utafanyika nchini Tanzania tarehe 22 Oktoba 2023 ukifuatiwa
na mkutano wa jukwaa la Majaji wakuu wa nchi hizo litakalofanyika tarehe 23-27
Oktoba, 2023 ambapo utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mtendaji
Mkuu alisema ajenda kubwa tatu zitakazojadiliwa kwenye Mkutano huo zitahusu marekebisho
na maboresho ya katiba ya chama, kuboresha mtandao wa chama hicho na mikakakti
ya masuala ya vyanzo vya fedha.
Aidha
alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Mahakama ya
Tanzania kutekeleza majukumu yake ipasavyo hususan kwa kuongeza rasilimali fedha na rasilimali watu. Aliongeza kuwa hivi sasa Mahakama inao watumishi zaidi ya
6000.
Mtendaji Mkuu amewashukuru na kuwapongeza Watumishi wa
Mahakama ya Tanzania kwa kuifanya Mahakama ya Tanzania kuwa ya kipekee.
Chama cha Watendaji wakuu wa Mahakama wa nchi zilizopo
kusini na Mashariki mwa Afrika (Southern and Eastern African Judiciary Administrators
Association- SEAJAA) kilianzishwa tarehe 30 Juni mwaka 2017 nchini Namibia.
Hadi sasa chama hiki kina wananchama kutoka nchi 13 ambazo ni Angola, Botswana,
Eswatin, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Sychells, Tanzania, Uganda, Zambia,
Zanzibar na Zimbabwe.
Malengo
ya kuundwa kwa chama hicho ni kubadilishana uzoefu katika nchi wananchama,
kuendeleza utawala wa sheria, kuongeza namna ya ushirikishanaji wa mambo
yanayotokea katika kila nchi wanachama ili kuongeza mbinu na mikakati ya
kutatia changamoto zinazoweza kutokea kwenye mnyororo wa utoaji haki.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Watendaji Wakuu wa Mahakama wa nchi zilizopo Kusini na Mashariki mwa Afrika, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungyumzana Waandishi wa Habari leo jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni