Alhamisi, 19 Oktoba 2023

WATENDAJI WAKUU WA MAHAKAMA KUSINI NA MASHARIKI MWA AFRIKA KUKUTANA JIJINI ARUSHA

Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Watendaji Wakuu wa Mahakama wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAJAA), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kikao cha watendaji hao kinatarajiwa kufanyika tarehe 22 Oktoba, 2023 katika Hoteli ya ‘Mount’ Meru jijini Arusha.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 19 Oktoba, 2023 jijini humo, Prof. Ole Gabriel amesema kwamba, kikao hicho kitajadili masuala ya Sheria na Utawala sanjari na kubadilishana uzoefu wa nchi moja na nyingine ambapo maazimio ya kikao hicho yatawasilishwa katika Jukwaa la Majaji Wakuu linalotarajiwa kufunguliwa na Rais Samia tarehe 23 Oktoba mwaka huu.

“Napenda kuwataarifa kuwa Tanzania imebahatika kuwa mwenyeji wa Kikao hicho sasa kitafanyika nchini Tanzania ambapo pia kitafuatiwa na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF),” amesema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, kikao hicho kitakuwa na ajenda kuu tatu ambazo zitajadiliwa katika mkutano huo nazo ni pamoja marekebisho ya katiba ya Chama hicho, kuboresha mtandao wa Chama hicho pamoja na kujadili mikakati ya kuongeza kipato.

Ameongeza kuwa, tangu kuundwa kwa chama hicho wamepata manufaa mbalimbali yakiwemo kuongeza mtandao, pamoja na kupata unafuu wa baadhi ya ada kwa wanachama.

Amesema kuwa, malengo ya kuunda Chama hicho ambacho kina miaka sita (6) sasa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kwa Nchi Wanachama, kuendeleza utawala wa sheria pamoja na kuongea namna ya ushirikishwaji wa namna ya kutatua changamoto mbalimbali za kisheria.

Ameongeza kuwa mpaka sasa, Chama hicho kina wanachama kutoka nchi 13 na jitihada zinaendelea kuhakikisha nchi tatu (3) zilizobakia zinajiunga na chama hicho. Nchi hizo ni Angola, Botswana, Eswatin, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Sychells, Tanzania, Uganda, Zambia, Zanzibar na Zimbabwe.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni