Alhamisi, 19 Oktoba 2023

NDEREMO, VIFIJO VYATAWALA MAPOKEZI YA MAGARI BUSEGA, ITILIMA

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mahakama ya Tanzania imekamilisha ahadi ya kuzipatia magari mapya Mahakama za Wilaya Busega na Itilima katika Mkoa wa Simiyu.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Busega, Mhe. Christian Rugumila na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Itilima, Mhe. Robert Kaanwa, wakiambatana na watumishi wa Mahakama hizo wamepokea magari hayo kwa furaha kubwa.

Kukabidhiwa kwa magari hayo kunajibu kilio cha muda mrefu katika Mahakama hizo cha changamoto ya usafiri kwa Viongozi hao wa Mahakama katika ngazi ya Wilaya.

Mahakama za Wilaya Busega na Itilima ni miongoni mwa Mahakama mpya 18 zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ambazo zilizinduliwa kwa pamoja tarehe 25 Novemba, 2022 katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Busega.

Kwa kipindi chote tangu kuzinduliwa kwa Mahakama hizo hakukuwa na usafiri wa wa uhakika wa kuwahudumia Mahakimu Wafawidhi hao, hasa wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza baada ya kupokea gari la Mahakama yake, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Busega alielezea kufurahishwa na hatua hiyo kwani amekuwa wakipitia changamoto nyingi, hasa wakati wa ukaguzi wa robo mwaka kwa  Mahakama za Mwanzo, kuhudhuria vikao vya kanda na katika kutekeleza majukumu ya ofisi kwa ujumla.

Naye Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Itilima hakuwa nyuma katika kuelezea furaha yake, kwani uwepo wa gari hilo unaenda kutatua changamoto nyingi zilizopo katika Wilaya hiyo kwa urahisi zaidi.

Kabla ya kupata magari hayo, Viongozi hao walikuwa wakiazima gari kutoka Mahakama ya Wilaya Bariadi kwa ajili ya shughuli za ukaguzi na kuhudhuria vikao mbalimbali vya kanda. Hatua hiyo ilipelekea wao kushindwa kukagua mara kwa mara maendeleo ya Mahakama za Mwanzo.

Wameushukuru uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa kwa kuwahudumia usafiri katika kipindi chote walichokua hawana gari.

Wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa ari zaidi kwani wameweza kurahisishiwa utekelezaji wa majukumu yao, hasa katika kuhakikisha wadaawa wa ndani na nje wanapata huduma bora.

 Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Itilima,Mhe. Robert Kaanwa (kulia) akikabidhiwa funguo na Dereva aliyeleta gari hiyo, Bw. John Masunga mbele ya watumishi wa Mahakama.

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Itilima wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea gari yao mpya.


Mapokezi ya gari mpya ya Mahakama ya Wilaya Busega.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni