Jumatano, 18 Oktoba 2023

JAJI MAGHIMBI AWAAPISHA WAJUMBE KAMATI YA MAADILI YA MAAFISA WA MAHAKAMA KIBAHA

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Kibaha Pwani

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewaapisha Wajumbe saba (7) wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Wilaya Kibaha, huku akiwaeleza kuzingatia kanuni ya tisa (9) ya Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237 kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha jana tarehe 17 Oktoba, 2023 katika hafla ya uapisho iliyofanyika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mhe. Maghimbi aliwakumbusha Wajumbe hao kuwa baada ya kiapo chao wanatakiwa kuzingatia Kanuni hiyo na pia wafanye majukumu yao bila upendeleo, chuki wala huba na kuzingatia miongozo ya Sheria husika. 

Kadhalika aliwaeleza wajumbe hao kuwa, Kamati hii kazi yake ni kujielekeza kwenye malalamiko, maadili ya watumishi wa Mahakama na si vinginevyo. 

Aidha, aliwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Alisema kwamba, Kamati hii ni lazima ijue mapana yake ya kazi na mipaka yake pia. Alihitimisha kwa kuwasisitiza kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao na kukaa vikao vya utendaji kazi kama inavyoelekezwa kisheria.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Maadili wa Maafisa wa Mahakama ngazi ya Wilaya  Kibaha na sehemu ya Watumishi wa Mahakama. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon na kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bw. Moses Magogwa.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akitoa maelekezo kabla ya kuwaapisha Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Wilaya ya Kibaha.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni