Jumatano, 18 Oktoba 2023

TOENI HUDUMA BORA YENYE KUJALI WATEJA; JAJI KADILU

Na Amani Mtinangi, Mahakama Kuu-Tabora

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu amewasisitiza Watumishi wa Kanda hiyo kutoa huduma bora, kujali wateja na kila mmoja kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Viongozi wa Mhimili huo.

Dkt. Kadilu alisema hayo tarehe 16 Oktoba, 2023 akiwa kwenye ziara ya kikazi Mahakama ya Wilaya Igunga, inayolenga kufanya ukaguzi wa Mahakama zilizopo chini ya Kanda hiyo.

“Kwanza niwapongeze sana kwa kazi kubwa mnayoifanya, kazi kubwa tuliyo nayo ni kumaliza mashauri; kazi hii inatupa wajibu wa kuhakikisha tunahudumia wadau na wadaawa wetu ambao wana matazamio fulani juu ya huduma tunazozitoa hivyo na sisi tunawajibika kusimamia majukumu yetu vizuri,” alisema Mhe. Dkt. Kadilu.

Akiwa katika Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Kadilu alijionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama, alipokea taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutawala na kiutumishi na kuongea na watumishi na wadaawa waliofika mahakamani. 

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe aliwapongeza watumishi wa Mahakama hiyo kwa namna wanavyoboresha utendaji kazi wao siku hadi siku huku akitoa mfano wa ujazaji wa rejesta za Mashauri ambao unazidi kuboreka.

“Kwa kweli niwapongeze sana watumishi kwa namna mnavyojaza rejesta za mashauri. Katika kaguzi zilizopita kulikuwa na mapungufu mengi ambayo kwa sasa yamerekebishwa kwa mfano kuandika jinsi shauri lilivyohitimishwa, kujaza nambari za risiti za wafungwa au ‘ERV’ kwa waliolipa faini, ninawasihi kuendelea hivyo hivyo,” alisema Mhe. Mwakatobe.

Katika ziara hiyo, Uongozi wa Kijiji cha Kazaroho ulitoa eneo lenye ukubwa wa takribani Hekari moja (1) kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. 

Akikabidhi eneo hilo Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Bw. Milambo Malila alisema kuwa wanalitoa eneo hilo kwa kutambua umuhimu wa huduma na kazi nzuri inayofanya na Mahakama. 

“Sisi kama Serikali ya Kijiji tulikaa na kuona umuhimu wa kuwa na Mahakama nzuri na ya kisasa, eneo hili ilipo Mahakama kwa sasa halitoshi kujenga Mahakama tunayoitaka ndio maana tumetoa eneo hili ili mtujengee Mahakama nzuri kabisa,” alisema Bw. Malila.

Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon alimshukuru Mwenyekiti wa Kijiji hicho na kuahidi kuanza taratibu za upimaji kwa ajili ya hatua zingine za umilikishwaji rasmi wa eneo hilo.

“Tunakushuku sana kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na Mahakama. Sisi tumelipokea eneo hili na tutalipima na kuendea na taratibu za kumilikiswa baada ya hapo hatua zingine zitaendelea,”.

Ukaguzi huo unaoendelea hadi tarehe 24 Oktoba, 2023 utajumuisha Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama zote za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo. 

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu akisaini kitabu cha wageni katika mojawapo ya vituo alivyotembelea katika ziara yake ya kikazi katika Kanda hiyo.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu (aliyesimama mbele katikati) akizunguma na Wadaawa wa Mahakama wakati wa ziara ya ukaguzi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kazaroho, Bw. Milambo John Malila (kushoto) akimuonesha Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon mipaka ya eneo lililotengwa kwa ajili ya Mahakama.

Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu (katikati) akiwasikiliza Wadau wa Mahakama akiwa katika ziara ya ukaguzi. Wa pili kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe, wa kwanza kulia Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Igunga, Mhe. Lydia Ilunda, wa kwanza kushoto ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Kundiata Maduhu  na wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Itumba, Mhe. Omary Abdallah.

Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon akitoa ufafanuzi wa mauala mbalimbali ya kiutumishi na kiutawala wakati wa kikao cha majumuisho ya ukaguzi wilayani Kaliua.


Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Ziba, Mhe. Goodluck Pallangyo akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Mwanzo Ziba.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni