Na. Paul
Pascal – Mahakama, Moshi
Uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi
umefanya mafunzo ya mfumo mpya wa
kielekitroniki wa kuratibu na kusimamia mashauri “Advanced
Electronic Case Management System (e-CMS)” ikijumuisha
watumishi na wadau wapatao 69 ikiwa ni pamoja na Mahakimu, Wahasibu, Wasaidizi
wa kumbukumbu, Mawakili wa Serikali na wa wakujitegemea.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja leo tarehe 18
Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Mhe. Omari Kingwele amesema, moja ya
mpango wa Mahakama, kupitia nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati wa miaka mitano
wa 2020/21-2024/25 ukihusisha lengo la kimkakati namba tatu linaelekeza kuwa “Kuongeza
ufanisi katika katika shughuli za kimahakama na kukuza matumizi ya TEHAMA”.
“Lengo hilo linaitaka Mahakama kuanzisha Mahakama
Mtandao (e-judiciary) ili kazi zote za kimahakama na utawala pamoja na huduma
zote zinazotolewa na Mahakama zitolewe ki-dijitali. Katika kutekeleza lengo
hili muhimu, Mahakama kwa kutumia wataalam wake wa ndani imejenga mifumo ya kielektroniki
itakayotumika kuratibu shughuli zote za kimahakama na zile za kiutawala”,
amesema Naibu Msajili.
Mhe. Kingwele amesema, mifumo hiyo inarahisisha na
kuboresha shughuli za utoaji haki kwa wateja wa Mahakama. Vilevile inatoa fursa
ya upatikanaji wa taarifa mbalimbali za utendaji wa kazi za Mahakama kwa
usahihi na kwa wakati.
Mahakama imekuwa na safari ndefu ya kufikia hatua
iliyofikia na ikumbukwe kuanzia mwaka 2014 Mahakama ilianza matumizi ya mfumo
wake maarufu wa JSDS toleo la kwanza hadi ilipofika mwaka 2018 ilihamia kwenye mfumo
wa JSDS 2.0 mfumo ukitoa huduma za kusajili mashauri kwa njia ya kielektroniki
(e-filing) na kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki (e-payment), ameongeza
Mhe. Kingwele.
“Watumishi wa Mahakama siyo wageni kwenye matumizi
haya ya kielektroniki. Kazi iliyo mbele yetu ni kuhakikisha kwamba Mahakama
inafikia viwango vya kimataifa kwenye matumizi ya TEHAMA na wanufaika wakubwa
wawe wateja wetu wa ndani na nje ya Mahakama”, amesisitiza Naibu Msajili huyo
Aidha, katika ujenzi wa mifumo yote ya kieletroniki
inayokwenda kufundishwa na wataalam wa Mahakama wamefuata miongozo, viwango na
taratibu zote kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao. Hivyo Mifumo
iliyojengwa imekidhi viwango vya kitaifa na kimataifa katika matumizi na
usalama wa taarifa zitakazoingizwa na kuhifadhiwa, amesema Mhe. Kingwele
Mhe. kingwele amewambia washiriki kuwa, ipo tofauti
kubwa kati ya mfumo wa “Judicial Statistical Dashboard Systema (JSDS 2.0)” na mfumo
mpya wa kielekitroniki wa kuratibu na kusimamia mashauri “Advanced
Electronic Case Management System (e-CMS)”. Mfumo wa
JSDS 2.0 ulitumiwa zaidi na wasaidizi wa kumbukumbu kusajili taarifa mbalimbali
za mashauri na kuziuhisha mara baada ya shughuli za usikilizaji wa mashauri
kukamilika mahakamani.
Mhe. Kingwele anasema, kwa kiasi kidogo Wahe. Majaji wafawidhi
na Mahakimu wafawidhi waliingia kwenye mfumo kupanga mashauri kwa Wahe. Majaji
au Mahakimu.
Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa “Advanced
Electronic Case Management System (e-CMS)” siyo tena
kwa ajili ya Makarani unakwenda kutumika kwa asilimia mia moja na Wahe. Majaji
na Mahakimu wote, hao ndiyo walengwa wakuu katika kuratibu shughuli zote
zitakazoendeshwa ndani ya mfumo huo na kwa lugha ya TEHAMA wanaitwa “ICT
users”.
“Niwaase wote mnaoshiriki mafunzo
haya mambo yafuatayo kuwa na mifumo mizuri ni jambo moja lakini kuitumia mifumo
hiyo ni jambo jingine lakini cha msingi sana, kama mifumo tutakuwa nayo halafu
hatuitumii kutatua matatizo yetu ama kurahisisha utendaji wetu kupitia mifumo
hiyo ni sawa na kutokuwepo”, Naibu Msajili aliwambia washiriki.
Lengo la haya mafunzo ni
kujua namna ya kuitumia mifumo hiyo kwa ufasaha, na kuwafundisha maafisa
wengine na watumishi wote pamoja na wadau kutumia mifumo hiyo kwenye utendaji
kazi wa kila siku ili kurahisha utoaji wa huduma.
“Ni matarajio ya viongozi
wetu kuwa, tutakwenda kuyafanyia kazi mafunzo haya na kuwafundisha wengine ili
kwa pamoja ifikapo tarehe Mosi Novemba, 2023 tuanze matumizi ya mfumo huu kama
ilivyoelekezwa ya kuwa ndiyo siku rasmi yakuanza kutumika katika mahakama zetu”,
amesisistiza Mhe. Kingwele.
Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Omari Kingwele akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa kielekitriniki wa kuratibu na kusimamia mashauri (hawapo pichani) leo tarehe 18 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Same Mhe Mussa Hamza (kushoto) ambaye ni muwezeshaji katika mafunzo hayo akiwa pamoja na wezeshaji wenza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Siha Mhe. Jasmine Abdul (kulia) wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Mhe. Omari Kingwele (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na
wahasibu kutoka Wilaya za moshi wanaoshiriki mafunzo hayo.
Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi Bw. Lukio Mrutu akiwa tayari kuwapitisha washiriki wa mafunzo hayo kwenye mfumo mpya huo.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni