Jumatano, 18 Oktoba 2023

UKARABATI WA JENGO JIPYA LA MAHAKAMA YA WILAYA MASWA MBIONI KUMALIZIKA

Na Naumi Shekilindi-Mahakama, Simiyu

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita jana tarehe 17 Octoba, 2023 ametembelea na kukagua maendeleo ya ukarabati wa jengo la Mahakama ya Wilaya Maswa mkoani hapa na kuhimiza kazi hiyo kukamilika haraka.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Bw. Kanyairita aliambatana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe Enos Missana, Mkaguzi wa Ndani, Bw. Kisasila Nsukuma na Mkandarasi wa jengo hilo, Bw. Emmanuel Kileo kutoka Kampuni ya Great Wall Construction Ltd.

Akizungumza katika kikao baada ya kutembelea jengo hilo, Mtendaji alimsisitiza mkandarasi kuzingatia tarehe aliyoahidi kukamilisha ujenzi ili jengo lianze kutumika haraka iwezekanavyo.

Kwa sasa Mahakama ya Wilaya Maswa inafanya kazi katika jengo la kukodi la shirika la posta lililopo wilayani hapo.

“Jengo hili litakapokamilika litaondoa gharama zinazotumika kulipa kodi katika jengo la kukodi, hivyo pesa hizo zitaweza kutumika kuendelea kukarabati na kutengeneza miundombinu katika Mahakama za Mwanzo zilizopo wilayani hapa,” alisema Bw. Kanyairita.

Sambamba na ukaguzi huo, Bw. Kanyairita alipita kuwasalimu watumishi wa Mahakama ya Wilaya Maswa na kuwasihi waendelee kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kufikia dira ya Mahakama ya utoaji haki kwa wakati.

Ukarabati wa jengo hilo ulianza tarehe 1 Agosti, 2022 na kutakiwa kuisha tarehe 30 Novemba, 2022, lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa nje ya uwezo, jengo hilo linatarajiwa kukamilika Oktoba, 2023.

Ukarabati wa jengo hilo unafanyika kutokana na fedha za za ndani, hii ni fahari kubwa kuona Mahakama inafanya juhudi ya kuwawezesha watumishi wafanye kazi katika mazingira mazuri na kutoa huduma bora kwa wateja.

Kazi ya ukarabati kwa sasa umefikia asilimia 89 na mkandarasi ameahidi kukamilisha ujenzi huo katika kipindi kifupi kijacho.

Mahakama ya Tanzania inatekeleza mkakati wake wa kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa ili kuimarisha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

 

Muonekano wa jengo la Mahakama kwa mbele.
Muonekano wa sehemu ya jengo la Mahakama kwa ndani.

Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Maswa kwa upande.

Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita (wa pili kushoto) akizungumza na wakandarasi pamoja na Mkaguzi wa Ndani wakati wa ukaguzi wa jengo hilo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni