Jumatano, 18 Oktoba 2023

WATUMISHI MAHAKAMA DODOMA, WANANCHI WAPIGWA MSASA KUHUSU KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

Na Arapha Rusheke-Mahakama, Kuu Dodoma

Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma pamoja na wananchi wametakiwa kutumia Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja (Call Center) cha Mahakama ya Tanzania kutoa maoni na malalamiko yao pale ambapo wataona hawajaridhika na huduma waliyopatiwa.

Wito huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Charles Mrema jijini hapa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma wakati wa ziara ya maafisa wa Call Centre kuzunguzia namna kinavyofanya kazi.

Alieleza kuwa Kituo chake kilianzishwa rasmi na Mahakama ya Tanzania tarehe 01 Machi, 2022 na hadi tarehe 30 Agosti, 2023 kimepokea jumla ya mirejesho 2,751 ikiwa ni maoni mapendekezo maulizo na malalamiko.

Jumla ya mirejesho 2,740 imefanyiwa kazi na wateja kupatiwa mrejesho, hii ni sawa na asilimia 98.6%, huku malalamiko 11 yanasubiria ufuatiliaji.

Alisema lengo la Kituo hicho ni kupokea mrejesho juu ya huduma zinazotolewa na Mahakama Tanzania nzima na kuhakikisha haki inatolewa kwa uwazi na uhakika kwa muda wote na kwa watu wote hapa nchini.

Mhe. Mrema aliongeza kuwa katika Kituo hicho wanatumia njia mbalimbali za upokeaji wa mrejesho kutoka kwa wateja kwa kutumia namba za simu 0752 500 400 na 0739 502 401 na kuhudumiwa moja kwa moja na watoa huduma waliopo. Simu hizo zinakuwa hewani kwa masaa 24 siku saba za wiki.

“Lalamiko ni siri, lazima lalamiko lichakatwe kwa usiri mkubwa hata afisa anayelalamikiwa asijue kuwa kuna lalamiko dhidi yake, hii huongeza imani kwa mtu aliyetoa taarifa,” alisema.

Kadhalika, Mhe Mrema alibainisha muda wa kushughulikia lalamiko kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa mteja (client service charter) ni siku saba na kama halijapata majibu kwa kipindi hicho msimamizi huliwasilisha sehemu husika.

Katika ziara hiyo ya siku mbili, Mhe. Mrema aliambatana na maafisa utumishi, Bi. Gladness Massawe na Bi. Angelina Agalla, wote kutoka Call Center.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Charles Mrema (wa kwanza kulia) ambae ni mwezeshaji mafunzo akiendelea kutoa mafunzo kwa wananchi (wateja) kuhusu utendaji kazi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Center) katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma. Kushoto ni Afisa Utumishi Gladnes Massawe.

Wananchi wakiwa wamekaa na kufuatilia kwa umakini mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Charles Mrema (aliesimama) akiendelea na mafunzo kwa watumishi wa Mahakama Dodoma.

Maafisa kutoka Call Center, Bi. Angelina Agalla (wa kwanza kulia) na Bi.Gladnes Massawe (wa kwanza kushoto) wakiwa wanatoa elimu kwa watumishi wa Mahakama na wananchi.

Sehemu ya wananchi waliohudhuria mafunzo.

Mwananchi alieonyesha kufurahishwa na mada hiyo, Bw. Yassin Adam akizungumza jambo wakati wa mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA, Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni