Jumatano, 18 Oktoba 2023

WANANCHI ARUSHA WAPATIWA ELIMU KUHUSU KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA

Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu, Arusha

Wananchi mkoani hapa, wakiwemo watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha hivi karibuni walipatiwa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja (Call Centre) cha Mahakama ya Tanzania.

Katika maelezo ya ufunguzi wa kipindi hicho, Msimamizi wa Kituo hicho, Bi. Evetha Mboya alisema huwa wanapokea mrejesho juu ya huduma zinazotolewa na Mahakama katika Mikoa yote ya Tanzania.

“Mrejesho huu ni pamoja na malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi toka kwa wateja. Wateja ni pamoja na watumishi wa Mahakama (wateja wa ndani) na wale wa nje (wananchi wanaopata huduma za Mahakama),” alisema.

Bi. Evetha aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho kumekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo, wananchi ambao ndio wadau wakubwa kupata sehemu ya kutoa madukuduku yao juu ya huduma za Mahakama.

Alisema pia kuwa Mahakama imeweza kujitahimini juu ya ubora wa huduma inayotolewa na kuweza kupata taarifa ya maeneo yanayolalamikiwa na kufanyiwa maboresho.

Aliyataja maeneo yanayolalamikiwa zaidi kuwa ni pamoja na mirathi, utekelezaji wa hukumu, dhamana na ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.

Aidha, Bi. Evetha alizitaja njia mbalimbali za kuwasilisha maoni, malalamiko, pongezi na mapendekezo, ikiwemo kwa mteja kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (sms) kwenda namba 0752 500 400 na 0739 502 401.

Kadhalika, alisema mteja anaweza kutumia email maoni@judiciary.go.tz, email maalum ya kupokea mrejesho unaohusiana na mashauri ya mirathi ccamirathi@judiciary.go.tz na njia ya tovuti ambayo ni www.judiciary.go.tz na mara baada ya kufungua tovuti hiyo, kuna kisanduku cha kutoa maoni juu ya huduma za Mahakama.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mwandamizi anayehudumu katika Kituo hicho, Mhe. Aden Kanje alieleza kuwa kama mteja hataweza kuwasilisha lalamiko lake Call Centre anaweza kupeleka lalamiko lake sehemu zingine.

Alizitaja sehemu hizo kama Kamari za Maadili za Maafisa wa Mahakama ngazi ya Wilaya na Mkoa, kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Mkoa au kwa Naibu Msajili na kwa kutumia mfumo wa malalamiko wa Sema na Mahakama.

Alieleza kuwa Kituo cha Huduma kwa Mteja kinazingatia mambo mbalimbali katika kuchakata malalamiko ya wateja, ikiwemo usiri na muda na kusisitiza kuwa lalamiko la mteja ni siri na lazima lichakatwe kwa usiri mkubwa kiasi kwamba hata afisa anayelalamikiwa hawezi kujua kama kuna lalamiko dhidi yake.

Alisema suala la muda ni muhimu, kwani lalamiko hushughulikiwa ndani ya siku saba na ikishindikana hupelekwa katika ngazi ya juu zaidi ili lipatiwe ufumbuzi na mteja hupatiwa mrejesho wa hatua iliyofikiwa katika kushughulikia lalamiko lake.

Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre) kilianzishwa na Mahakama ya Tanzania tarehe 01 Machi, 2022 chini ya Kurugenzi ya Huduma za Kimahakama, Ukaguzi na Maadili kwa lengo la kupata mrejesho toka kwa wateja wa Mahakama juu ya huduma zinazotolewa.

Kituo hiki ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama, hasa nguzo ya tatu ambayo ni “ushirikishwaji wa wadau na kujenga imani kwa wananchi.”

Tangu kuanzishwa kwa Kituo hiki, Mahakama ya Tanzania imepata manufaa makubwa kwani hadi kufikia tarehe 30, Agosti 2023, kituo kimeweza kupokea jumla ya mirejesho 2,751 ikiwa ni maoni, mapendekezo, maulizo, malalamiko na pongezi. Mirejesho 2740 tayari imefanyiwa kazi na wateja kupatiwa mrejesho, sawa na asilimia 98.6 na malalamiko 11 yanaendelea kushughulikiwa.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Aden Kanje (juu na chini) akitoa elimu kwa wateja na watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Kulia ni msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Bi. Evetha Mboya.

Mwananchi (mteja) akiuliza swali kuhusu kituo cha huduma kwa mteja mkoani Arusha.
Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na watoa elimu wa Kituo cha Huduma kwa Mteja mkoani Arusha.
Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja, Bi. Evetha Mboya akigawa vipeperushi kwa wananchi wakati wa utoaji wa elimu kuhusu huduma zitolewazo na Kituo hicho.

Baadhi ya wananchi waliopata elimu kuhusu huduma zitolewazo na Kituo cha Huduma kwa Mteja katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni