Jumanne, 17 Oktoba 2023

MAANDALIZI YA MKUTANO ‘SEACJF’ YASHIKA KASI

  • Waandishi mkoani Arusha wapigwa msasa kuhusu Jukwaa hilo

Na Seth Kazimoto, Mahakama Kuu Arusha

Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) leo tarehe 17 Oktoba, 2023 imefanya semina fupi kwa Waandishi wa Habari mkoani Arusha iliyolenga kuwapa elimu  kuhusu Jukwaa hilo ili waweze kuandika kwa ufasaha na kusaidia kuufahamisha umma juu ya Mkutano huo unaotarajia kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi  27 Oktoba, 2023 jijini humo.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amesema kupitia mkutano huo Mkoa wa Arusha na nchi kwa ujumla utapata faida mbalimbali kama vile mkoa kujulikana kimataifa, kuwakutanisha Viongozi wa Mahakama wa Ukanda wa Afrika na kuitangaza nchi kiuchumi hususani katika suala la utalii. 

“Lengo la Jukwaa la Majaji Wakuu ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya Kisheria ili kurahisisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo. Hii ni pamoja na kuhakikisha zinakuwepo Sheria mbalimbali zitakazowezesha ufanyaji biashara baina ya nchi za Ukanda wa Afrika, kusikiliza na kutatua migogoro ya biashara kisheria na hatimaye kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi hizi kutokana na ukweli kwamba wafanyabiashara watafanya kazi zao kwa wepesi zaidi,” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.  

Aidha, Mhe. Kihwelo amewaeleza Wanahabari hao kuwa Kaulimbiu ya Mkutano huo ni; Wajibu wa Mahakama za Kitaifa katika utatuzi wa Migogoro kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA): Matumizi ya Teknolojia ya Kisasa ili kuongeza  Ufanisi Katika Utoaji Haki.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya Teknolojia za kisasa, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema yanasaidia kutatua migogoro hiyo kwa wakati na hivyo kuongeza kasi ya mahusiano ya biashara na uwekezaji. 

Jaji Kihwelo alitaja baadhi ya manufaa ya uwepo wa Jukwaa la Majaji Wakuu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwepo na kuimarika kwa jukwaa hili tangu kuanzishwa kwake, kukua kwa mahusiano baina ya nchi wanachama wa Jukwaa, kubadilishana uzoefu katika utatuzi wa migogoro katika nchi wanachama na pia kubadilishana uzoefu katika namna bora ya usimamizi na uendeshaji wa Mahakama.

Akitoa mada ya Itifaki, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amevisisitiza Vyombo vya Habari mkoani humo kuzingatia uzalendo katika  uandishi wa Habari pamoja na kuzingatia itifaki wanapotekeleza majukumu yao katika kipindi chote cha mkutano. 

“Ninyi ni kiungo muhimu katika jamii na mna mchango mkubwa, ni muhimu mnapotekeleza majukumu yenu kuhakikisha mnatunza usalama wa Taifa kwa kuepuka kuandika habari za upotoshaji, kutunza hadhi ya Viongozi wa kitaifa, kushirikiana katika kupeana taarifa sahihi za mkutano huo na lengo lao liwe ni kuhabarisha umma na sio kujipatia kipato,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Mkutano huu unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na utahudhuriwa na Majaji Wakuu 16 na wajumbe mbalimbali. Aidha, mada mbalimbali zitatolewa na Wanazuoni na Wanasheria waliobobea ambao ni Majaji Wakuu Wastaafu wa Nchi wanachama wa Jukwaa hili ambao wanatarajiwa kuwapa uzoefu wa kisheria Viongozi wa sasa na kushauri namna bora ya kusimamia na kuendesha Mahakama.

Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika lilianzishwa mwaka 2003 na makao yake makuu yapo Lusaka Zambia. Itakumbukwa kwamba mkutano wa Jukwaa hili kwa mwaka jana ulifanyika nchini Msumbiji. 

Nchi zinazotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na Angola, Zambia, Botswana, Eswatin, Kenya, Uganda, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Mauritius na Shelisheli. 

Kadhalika, wakati Mkutano huo ukiendelea kutakuwa pia na maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za hapa Tanzania, baadhi ya  Taasisi zitakazoshiriki ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na majini (LATRA), Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na Chuo Kikuu Mzumbe na nyingine kadhaa.

Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe.  Dkt. Paul Kihwelo (katikati) akifafanua jambo wakati wa kikao na Waandishi wa Habari mkoani Arusha uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha leo tarehe 17 Oktoba, 2023. Kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga na kulia ni Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza wakati wa Mkutano kati ya Mahakama na Waandishi wa Habari mkoani Arusha uliofanyika leo tarehe 17 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mtendaji Mkuu  Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) wakati wa kikao na Waandishi wa Habari kilichofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha leo tarehe 17/10/2023. Katikati ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu  Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga.

Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Arusha wakishiriki kikamilifu katika kikao cha maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu utakaofanyika tarehe 23-27 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa 'Mount' Meru jijini Arusha. 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni