Jumanne, 17 Oktoba 2023

JAJI RWIZILE ATEMBELEA OFISI YA MKUU WA WILAYA UVINZA

Asisitiza ushirikiano kati ya Mahakama na Serikali

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amemtembelea Mkuu wa Wilaya ya Uvinza lengo likiwa ni kukuza mahusiano kati ya Serikali na Mahakama.

Akizungumza hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mhe. Dinnah Mathamani, Jaji Mfawidhi alisema kuwa pamoja na mambo mengine ziara hiyo ina lengo la kufahamiana kwani tangu ateuliwe kusimamia Kanda hiyo ndio mara yake ya kwanza kufika katika Wilaya hiyo.

“Tunakupongeza kwa ushirikiano unaoendelea kutupatia Mahakama ukiwa kama Mwenyekiti na mlezi wa maadili ya Maafisa wa Mahakama, tunatarajia ushirikiano zaidi ili kuimarisha na kurahisisha shughuli za Mhimili katika kusimamia maadili ya Maafisa wa Mahakama katika eneo  lako,” alisema Jaji Rwizile.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinnah Mathamani, alisema Mahakama ni mdau mkubwa wa Serikali hivyo amefurahishwa kwa ujio huo wa Jaji Mfawidhi na Viongozi Waandamizi wa Mahakama Kanda ya Kigoma.

Aliongeza kuwa sasa, ametekeleza ahadi aliyompa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof Ibrahim hamisi Juma wakati wa ziara yake na Tume ya utumishi wa Mahakama ya kumpatia nyumba Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa changamoto zilizowasilishwa wakati wa ziara hiyo mwezi Juni, 2023.  

“Tutaendelea kushirikiana kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Mahakama ikiwemo miundombinu ya umeme na makazi ya watumishi kwa sasa ninatimiza ahadi niliyompa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kumpatia nyumba Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Uvinza, Mhe. Misana Majula”. Alisema Mhe. Mathamani.

Upande wake Naibu Msajili, Mhe. Gadiel Mariki, alimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ahadi zake kwa Mahakama zilizopo katika Wilaya yake huku akisema kuwa, endapo zikitatuliwa zitasukuma mbele kasi ya kusikiliza mashauri yaliyopo mbele ya Mahakama hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rwizile aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw.Benjamin Mlimbila na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Misana Majula Mwenyeji wa Wilaya hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile(kulia) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinnah Mathamani mara baada ya  Jaji huyo kuwasili katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo hivi karibuni.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile, akisaini  kitabu cha wageni alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Uvinza hivi karibuni.


Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinnah Mathamani akimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (hayupo katika picha) alipotembelea Ofisi hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kigoma Mhe. Gadiel Mariki, akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Uvinza hivi karibuni.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni