Na. Hilary Lorry
Mahakama, Lindi
- Afurahishwa na kiwango cha ujenzi uliofanywa na kampuni ya Uandisi ya Kiure.
- Avutiwa na ubora na mwonekano wa Samani zilizotengenezwa kwa ustadi na ubora wa hali ya juu.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Mbeyela akabidhiwa
jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Liwale na Kampuni ya Uhandisi ya Kiure
mara baada ya kukamilika kwake.
Akizungumza wakati wa zoezi la makabidhiano hayo tarehe
10 Oktoba, 2023 Mtendaji huyo Bi. Mbeyela alisema, kampuni ya Uandisi ya Kiure
imefanya kazi iliyopewa kwa weledi na ufanisi mkubwa na kuhakikisha kuwa jengo la
Mahakama ya Wilaya ya Liwale linakamilika katika viwango vilivyokubaliwa kwenye
mkataba kwa ubora unaotakiwa.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri
mliyoifanya ubunifu unaonekana na juhudi kubwa ya kukamilisha kazi hii kwa
kiwango kizuri na kutuwezesha makabidhiano haya kufanyika leo ya jengo la
kisasa la kutolea huduma ya haki kwa wananchi likiwa katika hali bora ya
kuridhisha na samani bora za kuvutia’’alisema Mtendaji Bi. Mbeyela.
Aidha, Mtendaji
Mbeyela alimpongeza Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA) Lindi pamoja na wasaidizi wake kwa usimamizi mzuri walioufanya katika
kuhakikisha jengo la Mahakama ya wilaya ya Liwale linakamilika katika kiwango
na ubora uliokusudiwa kwa kuzingatia
matakwa ya mkataba wa ujenzi huo.
Wakielezea kwa nyakati tofauti Meneja wa kampuni ya Uandisi
ya Kiure Mhandisi Bw. Juma Mkwawa
na mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Lindi Mhandisi
Mshauri Bw. Greyson Kanyaburugo waliupongeza
Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi na viongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Mtwara kwa uongozi mzuri na ushirikiano wa karibu
waliouonyesha katika kipindi chote cha ujenzi jambo ambalo limerahisisha jukumu
zima la kukamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Liwale katika ubora uliokusudiwa.
Zoezi la Makabidhiano ya Jengo jipya la Mahakama ya
Wilaya ya Liwale limefanyika kati ya Kampuni ya Uandisi ya Kiure ambao ni
wajenzi wa jengo hilo, Kaimu Meneja wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni Mhandisi
mshahuri wa ujenzi na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.
Katika ziara hiyo ya kukabidhiwa jengo Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi. Mbeyela aliongozana na Afisa utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bw.Stephano Morey, Afisa Utumishi Mahakama ya Wilaya ya Liwale Bi. Neema Nyakaka.
Mwonekano wa Jengo jipya la kisasa Mahakama ya Wilaya ya Liwale.
Mhandisi Mshauri wa Wakala wa Majengo
Lindi Bw. Grayson Kanyaburugo (mwenye shati
la dark blue) akipokea hati ya makabidhiano ya kukamilika kwa jengo kutoka kwa
Mhandisi Juma Mkwawa (kushoto) kutoka kampuni ya Uandisi ya Kiure huku Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip Mbeyela
akishuhudia makabidhiano hayo.
Afisa Utumishi Mahakama ya Hakimu Mkazi
Lindi Bw. Stephano Morey aliyenyoosha mikono akitoa neno la pongezi
kwa kazi nzuri waliyofanya kampuni ya Uandisi Kiure pamoja na wakala wa
majengo Lindi katika kuhakikisha jengo linakabidhiwa katika ubora unatakiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni