Alhamisi, 12 Oktoba 2023

WADAU HAKI JINAI SINGIDA WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA WA KURATIBU MASHAURI MAHAKAMANI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa ametoa rai kwa wadau wa Mahakama kuufahamu na kuutumia Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri mahakamani (Advanced Case Management System) ili kwenda sambamba na azma ya Mhimili huo ya kutotumia karatasi ‘paperless court’.

Akizungumza leo tarehe 12 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama hiyo wakati akifungua Mafunzo ya Mfumo huo kwa Wadau, Mhe. Nzowa amesema ni muhimu waufahamu vizuri kwakuwa utapunguza matumizi ya karatasi mahakamani na ni rahisi kwa watumiaji.

“Ndugu wadau wa Haki Jinai ni lazima kuufahamu mfumo huu vizuri kwani mfumo huu umepunguza matumizi ya karatasi mahakamani, jiandaeni kujifunza na kuelewa mfumo huu vizuri,” amesema Mhe. Nzowa.

Naye, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo ambaye ni Afisa TEHAMA, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bi Amina Ahmad amewaeleza wadau kuwa, Mfumo huo ni mzuri zaidi na una maboresho ukilinganisha na ule wa awali kwani umeweza kusomana na Taasisi zingine na hivyo, kurahisisha kazi kwa kila mmoja.

Aidha, Bi. Amina amewajulisha Wadau hao kwamba, Mfumo huo utaanza rasmi tarehe 01 Novemba, 2023 hivyo amewaomba kutoa ushirikiano na kuwa tayari kujifunza na kuutumia.

Mfunzo haya yamehudhuriwa na Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, Wanasheria kutoka Magereza, TAKUKURU pamoja na Waendesha Mashtaka kutoka Wilaya za Iramba na Manyoni.

Mwezeshaji wa Mafunzo ambaye ni Afisa TEHAMA, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke, Bi. Amina Ahmad (aliyesimama mbele) akiwasilisha mada kuhusu Mfumo Mpya wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri Mahakamani (Advanced Case Management System) kwa wadau wa Haki Jinai mkoani Singida leo tarehe 12 Oktoba, 2023.

Sehemu ya Wadau wa Haki Jinai mkoani Singida wakimsikiliza Mtoa Mada, Bi Amina Ahmad (aliyesimama mbele yao).

Afisa TEHAMA, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia -Temeke, Bi. Amina Ahmad  akiwaelekeza kwa vitendo sehemu ya wadau walioshiriki katika mafunzo ya Mfumo Mpya wa Usajili na Usimamizi wa Mashauri Mahakamani (Advanced Case Management System).

Mtendaji Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo. Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni