Jumapili, 22 Oktoba 2023

MAANDALIZI YA MKUTANO “SEACJF” YAPAMBA MOTO

 ·       KAMATI YA ITIFAKI NA MAPOKEZI YANOLEWA

 Na Seth Kazimoto - Mahakama Kuu Arusha

Kamati ya maandalizi ya mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika “SEACJF” imefanya mafunzo ya Itifaki na mapokezi kwa kamati ili kuwapa wanakamati hao uwezo wa kutekeleza  majukumu yao wakati wote wa mkutano.

Akifungua mafunzo hayo kwa wajumbe wa Kamati ya Itifaki na Mapokezi mwishoni mwa wiki jijini Arusha, Mkurugenzi wa Utwala na Rasilimali watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick alisema mafunzo hayo yatawezesha wanakamati hao kutimiza wajibu wao kwa kufuata taratibu zinazotakiwa na hatimaye kufanikisha mkutano kwa ufanisi wa hali ya juu.

’’Mafunzo haya yatajikita kwenye maeneo ya itifaki, mapokezi na tabia njema na kuwataka wanakamati wote kushiriki kikamilifu ili kila mmoja aelewe anayopaswa kufanya kwa wakati sahihi na kwa namna inayofaa’’.

Akitoa mada ya Itifaki, Mapokezi na Tabia njema, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Mahakama ya Tanzania Bw. Stephen Magoha alieleza kuwa Itifaki ni taratibu zinazoongoza na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali, hususani za kiserikali na kidiplomasia na sababu ya kuwa na taratibu hizi ni kuweka miongozo mahsusi na utaratibu maalum utakaofuatwa katika kufanya mambo mbalimbali.

Bw. Magoha alisisitiza umuhimu wa wanakamati kufahamu muundo wa vyeo vya viongozi na jinsia zao, upangaji wa magari ya viongozi, muundo wa ujumbe, kujua idadi ya watu wanaosafiri,  kufanya maandalizi ya malazi, kujua sehemu au nafasi (kiti) atakapokaa mgeni, kuandaa eneo la chakula na kupanga mazingira ya eneo la mkutano.

Aidha, akizungumzia suala la tabia njema, Bw. Magoha alisema kuwa ni vigezo ambavyo Afisa itifaki anapaswa kuwa navyo kwani tabia za kiitifaki zinasisitizwa pia kwa watumishi wa Umma, ambao kwa nafasi walizonazo huwa ndio kioo cha serikali. Alitoa mfano wa tabia hizo kuwa ni pamoja na namna ya kuzungumza na viongozi, matumizi ya kistaarabu ya simu za mikononi, ustaarabu wa mezani wakati wa chakula na uvaaji wa mavazi ya heshima na yenye staha.

Mafunzo haya ni sehemu ya mandalizi ya Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika “SEACJF” unaotarajiwa kesho tarehe 23 Oktoba, 2023 na kumalizika Oktoba 27 katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Wajumbe wa kamati ya Itifaki na Mapokezi wakipatiwa mafunzo ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika kujiandaa na Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika “SEACJF” yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano IJC Arusha.

 

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akifungua mafunzo ya Itifaki kwa wanakamati wa Itifaki na Mapokezi ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika “SEACJF” yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano IJC Arusha. 

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha akitoa mada kwa wanakamati ya Itifaki na Mapokezi kwa ajili ya Maandalizi ya Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika “SEACJF” yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano IJC Arusha. 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni