Jumatatu, 23 Oktoba 2023

WATENDAJI WAKUU 'SEAJAA' WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Watendaji Wakuu wa Mahakama kutoka nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAJAA) wamekutana kujadili na kujiwekea mikakati ya kuboresha mnyororo wa utoaji haki katika nchi hizo ikiwemo kusimamia upatikanaji wa haki kwa wakati.

Akizungumza katika Mkutano mkuu wa Chama hicho jana tarehe 22 Oktoba, 2023 jijini Arusha, Mwenyekiti wa watendaji wakuu wa Mahakama wa nchi hizo (SEAJAA), Prof. Elisante Ole Gabriel alisema lengo mahsusi la mkutano huo ni kujiwekea mikakati ya jinsi gani mnyororo wa utoaji haki katika nchi zetu hizo unatakiwa kuwa.

"Sisi kama Watendaji Wakuu wa Mahakama tuna wajibu mkubwa wa kusaidia katika mnyororo wa utoaji haki wa nchi hizi wanachama unatolewa kwa tija. Kikubwa tunachosisitiza ni kuhakikisha kwamba ule mnyororo wa haki unakua bora, wenye tija lakini pia upatikane kwa urahisi zaidi bila kucheleweshwa,” alisema Prof. Ole Gabriel.

Aliongeza kwa kusema kuwa, “Kama ambavyo tunafahamu mara zote haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa kwa hiyo ningependa katika hizi nchi wanachama kama watendaji tuchangie vizuri zaidi katika kuboresha utoaji wa haki.”  

Kadhalika, Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa, katika Mkutano wao wanalenga pia kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya nchi wanachama ili ikibidi nchi zote za Afrika ziweze kujiunga na Chama hicho.

“Kikao hiki kitatupa pia fursa ya kujitathmini tulipotoka na tunapotaka kwenda ikiwa ni pamoja na kujadili mipango ya kuongeza idadi ya wanachama,” alieleza.

Kuhusu mahusiano baina ya nchi hizo, Prof. Ole Gabriel alisema, kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kikao hicho wanatumia fursa hiyo kutangaza utendaji kazi wa Mahakama ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria wa Mahakama ya nchini Shelisheli, Bw. Lionel Garrick alisema kupitia kikao hicho wameweza kubadilishana uzoefu baina ya nchi kwa nchi na itawaongezea uelewa zaidi katika utendaji kazi wao wa kila siku.

Mkutano huo wa ‘SEAJAA’ umetanguliwa na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (SEACJF) unaoanza leo tarehe 23 Oktoba mwaka huu katika ukumbi wa ‘Mount’ Meru jijini Arusha ukilenga kujadili kwa kina na kuangalia masuala ya kuboresha katika huduma ya utoaji haki kwa nchi hizo.



Watendaji Wakuu wa Mahakama 13 kutoka nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAJAA) wakiwa katika Mkutano wao mkuu wa mwaka uliofanyika jana tarehe 22 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha. Aliyeketi mbele ni Mwenyekiti wa 'SEAJAA',  Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mwenyekiti wa watendaji wakuu wa Mahakama wa nchi hizo (SEAJAA), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Watendaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAJAA) (hawapo katika picha) alipokuwa akifungua Mkutano wao Mkuu wa mwaka uliofanyika jana tarehe 22 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.
Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano huo wakifuatilia kinachojiri.
Mmoja kati ya Wanachama wa 'SEAJAA', Mhe. Boikobo Keaikitse akizungumza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa  'SEAJAA' uliofanyika jana tarehe 22 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.
Mwenyekiti wa watendaji wakuu wa Mahakama wa nchi hizo (SEAJAA), Prof. Elisante Ole Gabriel  (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji Wakuu kutoka Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEAJAA) mara baada ya Mkutano wao uliofanyika jana tarehe 23 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni