Jumatatu, 23 Oktoba 2023

MAFUMO MPYA WA MASHAURI WAPOKELEWA VYEMA MUSOMA

Na Francisca Swai, Mahakama - Musoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, imefanya mafunzo elekezi juu ya matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu na kusimamia mashauri mahakamani ‘Advanced Electronic Case Management System (e-CMS)’ kwa watumishi na wadau mbalimbali wapatao 60.

Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley, akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama hiyo, alisema mfumo huu umeletwa mahsusi ili kusaidia na kuongeza kasi katika usikilizwaji wa mashauri ikiwepo upatikanaji wa taarifa muhimu kwa usahihi na kwa wakati.

Aidha, Mhe. Erick Marley, amewasisitiza Mahakimu kuendelea kufanya mazoezi mara kwa mara ya namna ya kutumia mfumo huu mpya ili pale utakapoanza rasmi tarehe Mosi Novemba, 2023, kusiwe na changamoto yoyote. 

‘Hii ni kutokana na namna mfumo huu ulivyo kuwa Wahe. Majaji na Mahakimu ndio wahusika wakuu katika matumizi ya mfumo huu tofauti na ilivyokuwa katika mfumo unaotumika sasa wa ‘Judicial Statistical Dasboard System (JSDS II)’ ambapo Wasaidizi wa Kumbukumbu ndio wahusika wakuu katika mfumo,”alisema. 

Naye Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Kanda ya Musoma, Bw. Simon Lyova, ameelezea maboresho makubwa yaliyofanywa katika mifumo mbalimbali ya Mahakama hasa mifumo ya kusajili na usikilizwaji wa mashauri kuanzia mwaka 2014, ulipoanza ‘Judicial Statistical Dasboard System (JSDS I)’, ikafanyiwa maboresho 2018 kuwa ‘Judicial Statistical Dasboard System(JSDS II)’ na sasa mwaka 2023 tunaanza mfumo mpya ulioboreshwa zaidi wa ‘Advanced Electronic Case Management System (e-CMS)’.

Bw. Simon Lyova amewaasa watumishi wa Mahakama na wadau wote kwa kupitia mafunzo hayo waendelee kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuwa tayari kuutumia.

Mafunzo haya yaliyolenga kuleta uelewa wa pamoja kati ya wajumbe hao, yamekuwa na ufanisi mkubwa kwani yamepokelewa vizuri, washiriki wameonesha uelewa mkubwa na utayari wa kuanza kutumia mfumo huo.

Mafunzo hayo elekezi yalihudhuriwa na watumishi na wadau mbalimbali ikiwemo Mahakimu, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Mawakili wa Serikali, Waendesha Mashtaka wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea, TAKUKURU na Magereza kutoka katika Wilaya zote sita za Mkoa wa Mara.

Washiriki wa mafunzo elekezi juu ya mfumo mpya wa mashauri wakisiliza na kufuatilia kwa makini maelezo ya matumizi ya mfumo huo, kutoka kwa Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley (aliyesimama mwenye tisheti rangi nyekundu).

Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Erick Marley, pamoja na Afisa TEHAMA Kanda ya Musoma, Bw. Simon Lyova, (waliosimama) wakishirikiana kujibu maswali mbalimbali ya wajumbe wakati wa mafunzo elekezi.


Afisa TEHAMA Kanda ya Musoma, Bw. Simon Lyova, akitoa maelezo na ufafanuzi juu ya maboresho mbalimbali ya mifumo iliyofanywa na Mahakama ya Tanzania wakati wa mafunzo elekezi yaliyofanyika Mahakama Kuu Musoma.

Afisa TEHAMA Kanda ya Musoma, Bw. Simon Lyova, akifanya mafunzo kwa vitendo kwa washiriki wa mafunzo elekezi yaliyofanyika Mahakama Kuu Musoma.

(Habari  hii imehaririwa na Magreth   Kinabo- Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni