Jumatatu, 23 Oktoba 2023

RAIS SAMIA AFUNGUA MKUTANO WA MAJAJI WAKUU JIJINI ARUSHA

 Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Tarehe 23 Oktoba, 2023 amefungua Mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo.

Ufunguzi wa Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Majaji wakuu 16 wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika ambazo ni Angola, Botswana, Eswatin, Kenya, Lesotho, Mauritius, Malawi, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika ya Kusini, Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Uganda na Zanzibar.

Miongoni mwa Viongozi wanaohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wakuu wastaafu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mabalozi, Mwakilishi wa Benki ya Dunia,  Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, na Naibu Makatibu wa Tume. Wengine waliohudhuria ni viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa.

Mkutano huo wa siku tano unaofanyika katika hotel ya Mount Meru unaongozwa na kauli mbiu inayosema wajibu wa Mahakama za Kitaifa katika utatuzi wa migogoro kwenye eneo huru la biashara la Afrika: Matumizi yta Teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Rais Samia aliwasili kwenye eneo la Mkutano majira ya saa nne asubuhi ambapo baada ya kuingia ukumbini ziliimbwa nyimbo tatu zikiwemo wimbo wa Taifa la Tanzania, wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wimbo wa Umoja wa Afrika.   

Baada ya nyimbo hizo zilifuata salaam za ukaribisho zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela na baadaye salaam za Jaji Mkuu wa Tanzania zikifuatiwa na hotuba fupi ya Mwenyekiti wa SEACJF, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Peter Shivute ambaye pia alimkaribisha Rais Samia kutoa hotuba.

Aidha, katika ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa SEACJF alimkabidhi Rais Samia zawadi zilizotolewa na Jukwaa hilo. Zawadi hizo ni picha inayoonesha Majaji Wakuu wa nchi za kusini na Mashariki mwa Afrika wakimpongeza Rais Samia kwa mchango mkubwa alioutoa katika maendeleo ya shughuli za utoaji haki, ikiwemo maboresho ya miundombinu ya Mahakama na matumizi ya Tehema yaliyorahisisha kazi ya utoaji haki.     

Pembezoni mwa Mkutano huo unaoendelea kuna maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi wadau wa Mahakama ya Tanzania. Baadhi ya  Taasisi zinazoshiriki ni pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA),  Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL).

Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika lilianzishwa mwaka 2003 na makao yake makuu yapo Lusaka nchini Zambia. Mwaka jana, Mkutano wa Jukwaa hili ulifanyika nchini Msumbiji. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili Hotel ya Mount Meru jijini Arusha tayari kwa kufungua Mkutano. wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika leo Tarehe 23 OIktoba, 2023.

Mwenyekiti wa Jukwaa Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Jamhuri  ya Namibia Mhe. Peter Shivute akimkabidhi zawadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo katika Hotel ya Mount Meru jijini Arusha. 

Sehemu ya Majaji Wakuu na wageni waalikwa wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.

Sehemu ya Wageni waalikwa wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Sehemu ya Majaji Wakuu na Wageni waalikwa wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.


Sehemu ya Wageni waalikwa wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.

Sehemu ya Wageni waalikwa wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika wakiwemo Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Naibu Makatibu.

Kikundi cha Nhgoma ya Asili kikitumbuiza kabla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni