Jumamosi, 14 Oktoba 2023

MAHAKAMA SPORTS YAJIZOLEA TENA NDOO, MEDALI SHIMIWI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) imekomba makombe matatu na medali tatu katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamehitimishwa leo tarehe 14 Octoba, 2023 mkoani hapa baada ya kushinda kwenye michezo mbalimbali.

Mahakama Sports imeshika nafasi ya pili kwenye mchezo wa Kamba Wanawake, ikashika nafasi hiyo pia kwenye Kamba Wanaume na nafasi ya pili kwenye Riadha Wanawake mita 3,000.

Kwenye Riadha Mahakama Sports pia imeshika nafasi ya pili mita 400 na nafasi kama hiyo kwenye kwenye mchezo wa Tufe na ikanyakua mshindi wa pili kwenye Bao.

Katika michezo ya Kamba na Bao Mahakama Sports ilikabidhiwa makombe kwa kila mchezo, huku washindi katika riadha na tufe wakivalishwa medali.

Kabla ya kukabidhiwa zawadi hizo kulifanyika michezo miwili ya fainali ya kuvuta kamba kwa Wanaume na Wanawake, huku Mahakama Sports ikikabiliana vilivyo na Ikulu na Uchukuzi, mtawalia, na kufanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kila mchezo.

Ulikuwa mchezo wa Kamba Wanawake ulioanza, huku Uchukuzi ambao walikuwa na nyuso tofauti na wale waliokuwa wamesajiliwa awali kushiriki kwenye mashindano hayo walifanikiwa kuwavuta Mahakama Sports kwenye mivuto yote miwili.

Baada ya mchezo huo kumalizika, ikafuata Kamba Wanaume iliyowashirikisha watoto wa Baba mmoja, Ikulu na Mahakama na mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili kwani katika mvuto wa kwanza hakuna aliyemtambia mwenzake.

Ikulu walifanikiwa kushinda katika mvuto wa pili baada ya viatu vya baadhi ya wachezaji wa Mahakama Sports kuchanika, hivyo kuwafanya wapoteze uimara wa kuhimili mchezo.

Akizungumza baada ya michezo hiyo ya fainali kumalizika, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema kuwa kazi iliyowaleta Iringa wameikamilisha na wametimiza kwa asilimia kubwa ahadi waliyokuwa wameitoa.

“Tuliahidi kurudi nyumbani na vikombe, nadhani umeona tumeshavichukua tayari  Kazi moja ikimalizika inaanzisha nyingine. Tutafanya tathmini kuangalia wapi tulipojikwaa ili turekebishe kwa ajili ya mashindano mengine yajayo,” amesema.

Katika mashindano hayo ya SHIMIWI yaliyoanza Septemba 29, 2023, Mahakama Sports ilishiriki katika michezo mbalimbali, ikiwemo Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe na Riadha.

Kwenye mchezo wa Kamba, Bao wanaume, Tufe na riadha imeshika nafasi ya pili kwenye kila mchezo, huku kwenye Netiboli na Mpita wa Miguu Wanaume ikashika nafasi ya nne, huku Karata ikiishia kwenye makundi.

Wachezaji wa Kamba Kamba Wanaume walioiwakilisha kwenye mashindano hayo walikuwa Leonard Kazimzuri, Joseph Chokela, Cletus Yuda, Luyuga Luyuga, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Abdulmumin Mbaraka, John Charles, Kumbukeni Mtete na Martin Mushi, Hemed Semith, Emmanuel Dasian, Ashel Chaula, Willy Mwaijibe, Mussa Komba na Marko Mochiwa.

Kwa upande wa Kamba Wanawake walikuwepo Judy Mwakyalabwe, Zahara Suleiman, Beatrice Dibogo, Melina Mwinuka, Rebeca Mwakabuba, Tumaini Kizito, Namweta Mcharo, Joyce Simba, Sarafina Mkumbo na Mariam Mayalla, Winiel Mahumbuga, Witness Lyasato, Veronica Rajabu, Eunice Lugiana na Janeth Mapunda.

Katika mchezo wa Netiboli, timu ilishika nafasi ya nne na Mahakama iliwakilishwa na Tatu Mawazo, Filomena Haule, Upendo Gustaf, Nyangi Kisangeta, Eunice Chengo, Sophia Songoro, Shan Ally, Agness Mwanyika, Nuru Nchimbi, Malkia Nondo, Talita Kayuli, Ruth Kibona na mchezaji kiongozi akiwa Theodosia Mwangoka.

Upande wa timu ya Mpira wa Miguu ambayo nayo imeshika nafasi ya nne, Mahakama iliwakilishwa na Fahamu Kibona, Michael Turuka, Nasoro Mwampamba, Gisbert Chentro, Rashid Mbwana, Akida Mzee, Kelvin Muhagama, Frank Obadia, Seleman Magawa, Martin Mpanduzi, Seif Shamte, Abdi Sasamaro, Emmanuel Mwamole, Juma Mbega, Davis Munubi, Timoth Mwakisamba, Gabriel Tabana, Nkruma Kitagile na Ramadhan Seif.

Timu ya Riadha iliundwa na Justa Tibendelana, Upendfo Gustaf, Mwajabu Bwire, Hemed Mtoa na Asante Nasary.

Benchi la ufundi liliongozwa na Kocha Mkuu Spear Mbwembe, Kocha Msaidizi Said Albea, Mwalinu wa Netiboli Paul Mathias, Timu Meneja Shaibu Kanyachole, Meneja wa Vifaa Eliya Ngule na Daktari Janeth Mapunda.

Viongozi ambao waliambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile, Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole na Mjumbe Rajabu Mwaliko.

Nahodha wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume Denis Kipeta akipokea kombe la mshindi wa pili kwenye mchezo huo.
Mahakama Sports Kamba Wanaume wakiwa na kombe lao.
Nahodha wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake Zahara Suleiman akipokea kombe la mshindi wa pili kwenye mchezo huo.
Mahakama Sports Kamba Wanawake wakisherekea ushindi na kombe lao.
Mshindi wa pili mchezo wa Bao Hashim Rashid akiwa na kombe lake.
Mshindi wa pili mchezo wa Tufe Martin Mushi (kushoto) akipongezwa baada ya kuvalishwa medali.
Mshindi wa pili riadha mita 3,000 Justa Tibendelana akivalishwa medali yake.
Mshindi wa pili riadha mita 400 Upendo Gustaf akivalishwa medali yake.
Shangwe kama lote baada ya kupokea vikombe na medali.
Hii hapa sehemu ya timu ya riadha iliyoiwakilisha Mahakama ya Tanzania.
Hii hapa sehemu ya timu ya Netiboli iliyoiwakilisha Mahakama ya Tanzania.
Hii hapa sehemu ya timu ya mpira wa miguu iliyoiwakilisha Mahakama ya Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni