Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mafunzo yaliyokuwa yanaendelea mjini hapa kuhusu
uendeshaji wa mashauri ya makosa ya wanyamapori na maliasili yamehitimishwa
jana tarahe 13 Oktoba, 2023.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba alisema wakati anahitimisha mafunzo hayo kuwa,
mafunzo hayo yaliandaliwa ili kukabiliana na changamoto za ushahidi hafifu ambao wakati mwingine unapelekea mshitakiwa
kuachiwa huru.
Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwajengea
uwezo maafisa wa Mahakama, wapelelezi pamoja na waendesha mashtaka ili wote wawe
na ufahamu wa kutosha kuhusiana na sheria husika.
Mhe. Chaba alisema pia kuwa mafunzo hayo yaliandaliwa
ili washiriki kuwaongezea ujuzi na maarifa katika kuyashughulikia mashauri hayo
kulingana na nafasi zao katika mnyororo wa utoaji haki hapa nchini.
Aidha, Jaji Chaba aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo kufanya
kazi kwa kuzingatia taaluma zao na kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa weledi
mkubwa katika utendaji wao wa kazi.
Aliwataka washiriki wote wajenge utamaduni wa kushirikiana
na wadau wengine muhimu katika maeneo yao ya kazi na watumie nafasi walizonazo
kujiendeleza kitaaluma ili kujifunza mambo mapya na kujiimarisha zaidi kiutendaji.
Kadhalika, Kaimu Jaji Mfawidhi aliwahimiza kuhakikisha
wanazingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika
kuboresha utendaji wa kazi zao.
“Katika mafunzo haya, nimejulishwa kuwa wamekuja
wataalamu wabobezi na na wakufunzi mahiri ambao wametoa mafunzo mahsusi
kuhusiana na uendeshaji wa mashauri ya makosa ya wanyamapori na maliasili. Ninaamini
washiriki wote tumepata msingi mzuri wa upelezaji, uendeshaji na usikilizwaji
wa mashauri ya wanyamapori.
“Mkumbuke kwamba, uendeshaji wa kesi yeyote ile hauna
tofauti na ujenzi wa nyumba ambapo huhitaji msingi ulio madhubiti ili kuhimili
misukosuko yoyote. Hivyo, mashauri yanayohusu wanyamapori yanahitaji wapelelezi
kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa, umakini wa hali ya juu sambamba na
kushirikiana na wadau muhimu,” alisema.
Mhe. Chaba alisema waendesha mashtaka nao wanapaswa
kuhakikisha mashauri ya aina hiyo yanaendeshwa kitaalamu na kwa weledi mkubwa kwa
kuwa ushahidi thabiti unaotolewa mahakamani ndiyo kitu pekee kinachoifanya
Mahakama kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hivyo, alisema suala la upelelezi na uendeshaji wa
mashauri ya aina hiyo ni muhimu katika utendaji wa haki kwa nafasi ya
wapelelezi na waendesha mashtaka.
“Endapo upelelezi utafanyika chini ya kiwango na kuwa
dhaifu, ni vigumu zaidi kwa waendesha mashtaka kuthibitisha kosa pasi na shaka
yeyote mahakamani na Mahakama kwa upande wake, haziwezi kutenda miujiza
kutokana na shauri husika kupelelezwa na hatimaye kufikishwa mahakamani wakati
ushahidi uliotolewa ni dhaifu au hafifu,” alisema Jaji Chaba.
Mhe. Chaba alisema kuwa anaamini mafunzo hayo
yamewanoa ipasavyo washiriki wote ambao idadi yao ilikuwa 160 na sasa wanakwenda
kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi ili kupunguza mauaji ya
wanyamapori ambazo ni nyara za Taifa.
Alisema, anaamini pia kwamba, washiriki wote
wamemaliza mafunzo yako kwa ufanisi mkubwa na kwamba wanaondoka wakiwa na ujuzi
tofauti na walivyofika kuhudhuria mafunzo hayo. Aliwaeleza washiriki kuwa
alivutiwa na mafunzo hayo kwa kuwa yalihusisha pia somo la maadili katika
utumishi wa umma.
Aidha, alisema kuwa Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza
mpango mkakati kupitia nguzo ya tatu, imeweza kuandaa mafunzo hayo kwa kuwashirikisha
wadau katika sekta ya upelelezi na waendesha mashtaka ikishirikiana na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto na wadau wengine (PLMS Foundation) katika kuwanoa
maafisa wa Mahakama na wadau wengine.
Naye Mratibu wa Mafunzo hayo, Mhe. Elimo Masawe
alisema kuwa mafunzo hayo yamefanikiwa kuwakutanisha wadau wa haki jinai,
kugawana uzoefu na kujadiliana changamoto wanazokutana nazo mara kwa mara
katika utendaji kazi kuhusiana na mashauri ya wanyamapori.
Alisema mada 17 zimefundishwa ambazo ziligusia mambo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya uhalifu tangu siku inapotolewa
mpaka siku ya mwisho ambapo adhabu hutolewa na Mahakama kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Masawe alisema kuwa, mafunzo hayo yamekidhi kiu
ya washiriki pamoja na kuangalia njia sahihi za kutanzua changamoto kubwa zilizopo
wakati wa upelelezi, uendeshaji na usikilizwaji wa mashauri ya wanyamapori.
Alisema anaamini ujuzi walioupata washiriki katika
mafunzo hayo, yataongeza ari na kasi ya ushughulikiaji wa mashauri hayo na hasa
ikizingatiwa kuwa uhalifu unabadilika mara kwa mara kulingana na teknolojia
inavyobadilika.
“Hivyo wapelele lazima wawe na ujuzi wa namna ya
kuchunguza uhalifu unaofanyika kwa kutumia teknolojia, jinsi ya kukusanya
ushahidi kwa misingi ya sheria na jinsi ushahidi utakavyotolewa Mahakamani.
Tusipopeana ujuzi wa kutosha waalifu watatuacha mbali,” alisema.
Alisema kuwa kesi ya uhalifu wa wanyamapori hata ikiwa
moja ni tatizo kubwa kwani mhalifu anapokamatwa na sehemu yeyote ya kiungo cha
mnyama ni ishara kuwa mnyama ameuwawa.
Mafunzo hayo yaliyofunguliwa tarehe 9 Oktoba, 2023
mjini hapa, yametolewa kwa washiriki 160 kutoka Mahakama ya Tanzania, Wapelelezi
na Waendesha mashtaka wa Serikali na yanategemewa kutolewa kwa awamu nyingine.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akizungumza wakati wa kufunga mafunzo
hayo.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la PAMS
Foundation, Bw.
Samson Kasala akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo ya
mashauri ya wanyamapori na maliasili mjini Morogoro.
Mratibu wa Mafunzo hayo,
Mhe. Ellimo Massawe akuzungumza wakati wa kufunga.
Washiriki wakikabidhiwa
vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo (juu na chini).
Washiriki (juu na chini) wakifuatilia
matukio mbalimbali wakati wa kufunga mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Iringa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni