Ijumaa, 13 Oktoba 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA KATAVI WAPIGWA MSASA ELIMU AFYA VIUNGO VYA MWILI

Na James Kapele-Mahakama, Katavi

Watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi leo tarehe 13 Octoba, 2023 wamepata elimu ya masuala ya afya ya macho, pua, masikio, na mfumo wa koo kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Katavi.

Shughuli hiyo imefanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu visababishi vya magonjwa yanayoathiri sehemu hizo muhimu za mwili wa binadamu na nanmna ya kujikinga na kisha kufanya vipimo bure kwa watumishi walioshiriki katika mafunzo hayo.

Madaktari bingwa waliongoza mafunzo hayo ni Dkt. Salome Renatus ambaye ni Mratibu wa Huduma ya Macho wa Hospitali ya Rufaa ya Katavi na Dkt. Noela Lema wa Kitengo cha Pua na Masikio katika hospitali hiyo.

Akizungumza wakati anatoa elimu ya macho, Dkt. Salome amesisitiza kwamba watumiaji wengi, hasa wa kompyuta wamekuwa wahanga wakubwa wa magonjwa ya macho kwa kuwa wengi hawajapa elimu ya nanma sahihi ya matumizi ya vifaa hivyo.

“Wengi wenu hapa mnatumia kompyuta na kila mtu anaitumia kulingana na namna macho yake yanavyotaka au meza na kiti anachotumia. Lakini nawashauri wekeni kompyuta zenu umbali wa urefu wa mkono wako ili mwanga usilete madhara ya moja kwa moja kwenye macho yenu,” alisema.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Afisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Bw. Ayubu Nyalobi ambaye alibainisha kuwa ofisi inatambua umuhimu wa watumishi kuwa na afya njema na ndiyo lengo la kuomba wataalamu hao wafike kufanya kazi hiyo.

Ameeleza kwamba ofisi itaendelea kuleta wataalam mbalimbali wa afya ili elimu kuhusu maeneo mbalimbali ya kiafya iwafikie watumishi, kwani ubora wa afya zao utaongeza ufanisi wa kazi na majukumu yao ya kila siku.

Pichani aliyesimama ni Dkt. Salome Renatus ambaye ni Mratibu wa Kitengo cha Macho Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Katavi. Aliyeketi ni Dkt. Noela Lema wa Kitengo cha Pua na Masikio kutoka katika hospitali hiyo.
Katika picha ni Dkt. Noela Lema akiwasilisha mada yake kuhusu afya ya Pua, Masikio na Koo kwa watumishi wa Mahakama waliohudhuria mafunzo hayo.
Pichani ni Sehemu ya watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi wakifuatilia mafunzo hayo. Aliyeketi wa kwanza kushoto n, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Mhe. Gosper Luoga.

Pichani ni aliyeketi ni moja kati ya watumishi wa Mahakaka, Bw. Josiah Mwalongo akipata vipimo katika baada ya mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni