Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mafunzo ya uendeshaji wa
mashauri ya makosa dhidi ya wanayamapori, ikiwemo ujangili yanayoendelea mjini
Morogoro yanazidi kupamba moto baada ya Majaji jana tarehe 12 Oktoba, 2023 kushika
usukani na kutoa darasa la namna bora ya uandishi wa hukumu.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali
ya PAMS Foundation yamezidi kuwajengea uwezo wadau wote katika myororo wa
utoaji haki nchini.
Mbali na washiriki toka
Mahakama ya Tanzania ambao ni Majaji na
Mahakimu lakini pia kuna waendesha mashtaka wa serikali pamoja na wapelelezi
ambao wote kwa pamoja wamekutana ili kuongeza ujuzi katika utendaji kazi.
Akitoa elimu ya uandishi
bora wa hukumu, mwezeshaji ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.
Mustafa Ismail alisema kuwa ni vyema wahakikishe kile wanachokiandika katika
hukumu zao kinawabainisha wao ni nani, uelewa wao na hata namna ya kuchanganua
mambo.
“Sio watu wote wamepewa
mamlaka ya kuhukumu, hivyo basi sisi tuliokasimiwa mamlaka haya tufanye kazi
kwa heshima kubwa na itubainishe ujuzi wetu,” alisema.
Washiriki wa mafunzo hayo
yaliyowajumuisha wadau 157 waligawanywa katika makundi matatu ambapo kundi la
kwanza lilipigwa msasa na Mhe. Ismail, kundi la pili lilinolewa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahimu
wakati katika kundi la tatu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam Mhe. Dkt Deo Nangela aliwafunda vyema washiriki hao.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwezile alifundisha washiriki hao kwa njia ya mtandao (Video Conference) akiwa kwenye kituo chake cha kazi na kueleza kwanini adhabu za vifungo zinatolewa, kanuni mbalimbali za adhabu na namna ya utoaji wa adhabu hizo.
Mwezeshaji ambaye ni Jaji
wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Mustafa Ismail akitoa somo juu ya namna ya
kuandika hukumu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahimu akiwanoa washiriki juu ya
somo la namna ya kuandika hukumu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt Deo Nangela akiwafunda washiriki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akifundisha kwa njia
ya mtandao (Video Conference) akiwa huko Kigoma huku washiriki wakifuatilia
kama inavyoonekana pichani.
Naibu Msajili, Mhe.
Ellimo Masawe ambaye pia ni mratibu wa mafunzo akiongea na washiriki kabla ya
kuanza kwa darasa kwa njia ya video.
Washiriki wakifuatilia darasa kwa njia ya Video Conference (juu na chini).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni