Ijumaa, 13 Oktoba 2023

MAHAKAMA SPORTS YAUNGANA NA WANAMICHEZO SHIMIWI KUFANYA MATENDO YA HURUMA IRINGA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Iringa

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) kwa kushirikiana na washiriki mbalimbali wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) leo tarehe 13 Octoba, 2023 wameungana na wanamichezo wengine kufanya matendo ya huruma kwenye vituo vinne vya watu wenye mahitaji maalum.

Uongozi wa SHIMIWI Taifa chini ya Katibu Mkuu Alex Temba uliongoza shughuli hiyo, huku Mahakama Sports ikiwakilishwa na wajumbe 12 akiwemo Katibu Mkuu Robert Tende. Vituo vilivyotembelewa ni Kituo cha Watoto Yatima Tosamaganga na vingine vya Ismani, Huruma na Furaha. Zawadi zilizotolewa zinajumla ya thamani ya shillingi 13,750,000.

Shughuli ya kutembelea vituo hivyo ilianza majira ya saa tatu na nusu hivi asubuhi kutokea katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha baada ya Viongozi wa SHIMIWI kuwagawa wanamichezo katika makundi manne kutokana na umbali wa vituo vilivyokuwa vimepangwa kutembelewa.

Mahakama Sports waliungana na wanamichezo wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Mifugo, Ras Mara na wengine kutembelea Kituo cha Tosamaganga, huku Katibu Mkuu SHIMIWI Alex Temba na Mratibu wa Masuala ya Kijamii Itika Mwankeja wakiongoza msafara huo.

Baada ya kuwasili katika Kituo hicho, wanamichezo hao walipokelewa na Mkuu wa Kituo Sister Hellena Kihwele ambaye aliwatembeza katika maeneo mbalimbali na kukutana na watoto.

Wanamichezo hao wameonesha upendo wa ajabu kwa watoto waliowakuta kwani walikuwa wanawagombania kuwabeba na kucheza nao michezo mbalimbali ya kitoto. Watoto walionekana kuwa na nyuso za furaha baada ya kuwaona wanamichezo hao.

Baada ya kuonesha upendo huo, Viongozi wa SHIMIWI na wanamichezo walikabidhi zawadi mbalimbali kwa Mkuu wa Kituo kwa niaba ya watoto.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Katibu Mkuu SHIMIWI alimweleza Sister Hellena kuwa zawadi hizo zinatokana na michango iliyotolewa na wanamichezo kutoka wizara, taasisi na idara mbalimbali ambazo zipo mkoani Iringa kwa ajili ya mashindano. 

"Tupo hapa Iringa kwa ajili ya mashindano yanayojumuisha watumishi wa umma kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Kabla hatujamaliza mashindano haya tumeamua kuja kuwaona watoto wetu kwa ajili ya kuwapa zawadi kidogo. Tumejichangisha kidogo kidogo kwenye posho zetu ili kupata zawadi hizi. Naomba uzipokee," amesema.

Naye mratibu wa masuala ya kijamii SHIMIWI amemweleza Mkuu wa Kituo kuwa zawadi ambazo wameziwasilisha zimezingatia makundi yote ya watoto, ikiwemo mchele, unga, sabuni, mafuta ya kula, maziwa, dawa za mswaki, miswaki, juice, madaftari na vingine vingi.

Amemwomba Sister Hellena kupokea zawadi hizo ili ziweze kusaidia ingawa kwa uchache ili watoto hao waweze kuvitumia. Kadhalika, Dada Itika alikabidhi fedha taslimu millioni moja kwa Mkuu huyo wa Kituo ili ziweze kusaidia katika mahitaji mbalimbali.

Akipokea zawadi hizo, Sister Hellena amewashuku Viongozi wa SHIMIWI na wanamichezo wote kwa moyo wa huruma waliouonesha kwa watoto hao. Amesema zawadi walizotoa kweli zimezingatia watoto wote waliopo kwenye Kituo chake, hivyo akashukuru kwa majitoleo hayo.

" Kwa mfano hapa tuna watoto ambao wametoka jeshini baada ya kumaliza mafunzo kwa mujibu wa sheria. Hawa ni wahitimu wa kidato cha sita na wamekulia hapa hapa. Tunasubiri mamlaka ziwapatie mikopo kwa ajili ya kwenda vyuoni. Kama hawatapata, basi nitakaa nao hapa hapa maana sina pa kiwapeleka" amesema.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Aines Kedimondi amewashukuru wanamichezo wote kwa kujitoa na kuomba makundi na watumushi wengine wa umma kuiga mfano huo kwa maslahi ya watoto na wenye uhitaji maalum. 

Sehemu ya wanamichezo kutoka Mahakama Sports, akiwemo Katibu Mkuu Robert Tende (wa tano kulia) walioshiriki kwenye matendo ya huruma.
Safari kuelekea Tosamaganga ilianzia hapa.

Sehemu ya Viongozi wa SHIMIWI na wanamichezo (juu na chini) wakiwa pamonja na zawadi walizotoa kwa watoto hao yatima.


Viongozi wa SHIMIWI wakikabidhi zawadi hizo kwa Masista wanaosimamia Kituo hicho. Picha chini Viongozi mbalimbali wakiwa na Masista hao.

Katibu Mkuu wa SHIMIWI Alex Temba (aliyebeba mtoto) akizunguza wakati wa kukabidhi zawadi hizo.
Mratibu wa Masuala ya Kijamii Itika Mwankeja (kushoto) akimkabidhi Sister Hellena Kihwele milioni moja kama sehemu ya zawadi hizo.
Afisa Ustawi wa Jamii Aines Kedimondi ( wa pili kulia) akitoa shukrani kwa zawadi hizo. Picha chini Sister Hellena Kihwele (katikati) akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo.

Mmoja wa watoto ambao wamekulia katika Kituo hicho akitoa shukrani kwa zawadi hizo.
Shughuli ya kuhamisha zawadi kwenda kuhifadhi sehemu salama inaanza huku Katibu wa Mahakama Sports Robert Tende akiongoza zoezi hilo.
Wanamichezo kutoka Mifugo pamoja na viongozi wa juu wa SHIMIWI (juu na picha mbili chini) nao hawakuwa nyuma.



Kabla ya makabidhiano ya zawadi kila mwanamichezo alionyesha upendo wa hali ya juu kwa watoto hao (juu na chini)

Safari ya kuanza kurudi kambini ilianzia hapa baada ya kutembelea Kituo hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni