Na Faustine Kapama – Mahakama.
Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye
pia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda ameeleza katika
taarifa yake aliyoitoa leo tarehe 16 Octoba, 2023 kuwa kuanza kwa mfumo huo
mpya ni sehemu ya maboresho yaliyofanywa na Mahakama katika maeneo mbalimbali.
"Lengo
la mfumo huu ni kuboresha upatikanaji wa huduma za haki kwa wakati na kwa
gharama nafuu. Moja ya maboresho hayo ni kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA katika
uendashaji wa shughuli zake, ukiwemo Mfumo wa Manejimenti ya Mashauri, yaani
JSDS2," ameeleza.
Kaimu Msajili Mkuu ameeleza katika taarifa hiyo
kuwa maendeleo hayo yanatokana na Mahakama kukamilisha ujenzi wa Mfumo huo
ambao unachukua nafasi ya JSDS2 iliyokuwa inatumika tangu mwaka 2018.
“Ujenzi wa mfumo huu unalenga kuongeza tija
katika shughuli za kimahakama, kupunguza gharama za kusikiliza mashauri kwa upande wa Mahakama na wananchi, kupunguza
muda wa kusikiliza mashauri na kusogeza zaidi huduma za kimahakama karibu na
wananchi,” ameeleza.
Amesema kuwa matumizi ya Mfumo wa e-CMS pia
yanalenga kutatua changamoto mbalimbali za JSDS2, zikiwemo kuongezeka kwa watumiaji
na matumizi ya mfumo huo usioendana na muundo wa awali wa mfumo na teknolojia
iliyotumika kuujenga na kutoruhusu mienendomya mashauri kuandikwa moja kwa moja
kwenye mfumo.
Mhe.
Kainda ameeleza kuwa Mfumo huo umekuja na muundo na teknolojia ya kisasa
inayoendana na mahitaji ya sasa ya Mahakama na wadau wake na inaweza kusomana na
mifumo mingine ya ndani ya Mahakama na ile ya wadau muhimu, wakiwemo Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka (NPS), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Dhamana (RITA) na Taasisi nyingine.
Kaimu
Msajili Mkuu huyo ameeleza katika taarifa yake kuwa hatua hiyo itarahisisha
upatikanaji wa taarifa muhimu kutoka katika taasisi na kuwawezesha wadau kupata
taarifa mbalimbali za mashauri kwa urahisi.
Amesema
mfumo huo mpya pia utarahisisha usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao,
upangaji wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu na utaruhusu mienendo ya
mashauri kuandikwa moja kwa moja kwenye mfumo na kuihifadhi kielektroniki.
“Katika Mfumo huo kuna
fomu maalum (template) za nyaraka mbalimbali zinazotumika mahakamani, zikiwemo
hati za shauri, hati za mashtaka, hukumu zitakazojazwa na watumiaji ndani ya
mfumo. Lengo ni kupunguza upakiaji wa nyaraka nyingi kwenye mfumo unaoweza
kuathiri utendaji wake,” Mhe. Kainda amesema.
Amesema Mahakama ya
Tanzania itakapoanza matumizi ya e-CMS, madirisha
yake ya msaada kwa wananchi (viosk) wasioweza kutumia mfumo huo mpya yanayotumika
kuwasaidia wananchi wasioweza kutumia wenyewe JSDS2 yataendelea kutumika pia.
Mahakama
ya Tanzania ilianza kupima e-CMS tarehe 2 Oktoba, 2023 katika Mahakama zote
nchini na zoezi hilo bado linaendelea. Mahakama inawaalika wananchi na wadau
wake kufungua mashauri ya majaribio kwa wingi kwenye mfumo huo unaopatikana
kupitia anuani ya https://cmstraining.judiciary.go.tz/.
Kipindi cha majaribio kitaendelea hadi tarehe 31 Octoba, 2023 kwa lengo la kupata changamoto zitakazojitokeza katika matumizi ya mfumo huo ili ziweze kufanyiwa kazi kabla ya kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huu hapo tarehe 1 Novemba, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni