Jumanne, 31 Oktoba 2023

MAHAKAMA YA WILAYA KWIMBA YAKABIDHIWA JENGO JIPYA

Na. Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza. 

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Nestory Mjunangoma amewataka watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba ambao ndiyo watumiaji wa jengo hilo kuhakikisha kuwa wanalitunza vizuri ili liweze kudumu kwa muda mrefu na hata huduma itakayotolewa iwe ni yenye kiwango cha juu kulingana na uzuri wa jengo hilo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo jana tarehe 30 Oktoba, 2023 mjini Ngudu Wilayani Kwimba, Mtendaji Mjunangoma alisema, ni fahari kwa Mahakama na wananchi kupata jengo la kisasa la kutolea huduma ya haki, hivyo watumishi wanadhamana ya kulilinda na kulitunza ili wananchi wapate huduma katika mazingira bora.

“Nawasihi kulitunza jengo hili ili iliweze kudumu kwa muda mrefu kwani kwa ujumla thamani ya Pesa iliyotumika hapa inaoneka wazi kwa uzuri na ubora wa jengo hili. Pia nategemea hata huduma zitakazotolewa humu zitakuwa bora zaidi kwani sasa mpo kwenye mazingira rafiki hivyo hata kazi zenu zitaendana na ubora na uzuri wa jengo hili.” alisema Bw. Mjunangoma.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kwimba Mhe. Dastani Ndeko alishukuru kwa kukabidhiwa jengo hilo na kutangaza rasmi kuwa huduma ndani ya jengo hilo zitaanza kupatika kuanzia tarehe 06 Novemba, 2023 ambapo yeye na watumishi wengine watakakuwa wameshahamia ndani ya jengo hilo.

“Naipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuweza kukamilisha ndoto za wana kwimba kwa kuweza kutupatia jengo hili. Kwa kuwa na jengo hili sasa litasaidia kuweza kusikiliza mashauri kwa wakati tofauti na hapo awali tulipokuwa tukichangia jengo na Mahakama ya Mwanzo Ngudu, lakini pia tulikuwa na uhaba wa vyumba vya kusikilizia mashauri. Kwa uwepo wa jengo hili jipya sasa Mahakimu wote tutakuwa na sehemu kwa ajili ya kuendesha mashauri na hivyo ile hali ya kusubiliana tena mmoja amalize ili mwingine atumie chumba haitokuwepo tena.” alisema Mhe. Dastan Ndeko.

Ujenzi wa Mahakama hiyo ulianza rasmi tarehe 22 February, 2022 na jumla ya shilingi za Kitanzania 1,106,414,827.50 zilitumika kuweza kukamilisha mradi huo wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kwimba ujenzi uliofanywa na Mkandarasi aitwaye Kampuni ya Uhandisi ya Kiure chini ya Msimamizi wa Majengo kutoka mamlaka ya ujenzi Tanzania (TBA) 

Nao, wananchi wilayani Kwimba mkoani Mwanza wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuweza kuwajengea jengo jipya kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya Kwimba na hivyo kuwawezesha kuendelea kuwa na imani na maamuzi yatakayokuwa yakitolewa ndani ya Mahakama hiyo.

Wakizungumza wakati wa tukio la makabidhiano ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kwimba lililojengwa na Kampuni ya Uhandisi ya Kiure chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Ujenzi Tanzania (TBA), wananchi hao walionekana kuvutiwa na uzuri wa jengo hilo la kisasa na lenye muenekano bora.

“Naishukuru Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Hamis Juma kwa kutujengea Wilayani kwetu jengo zuri hili ambalo tunaamini pia ndani ya jengo hili mashauri yetu yatasikilizwa kwa wakati na haki itapatikana kwa wakati kwa kuzingatia sheria za Nchi.” alisema Bw. Mayunga Manyilizu.

Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya wilaya Kwimba lililokabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania jana tarehe 30 Oktoba 2023, tukio lilifanyika mjini Ngudu na kuhudhuliwa na watumishi mbalimbali wa Mahakama na wananchi wa Kwimba (hawapo pichani).

Msanifu Majengo kutoka TBA, Bi. Suzanne Bonaphace akikabidhi funguo za jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kwimba kwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Bw. Nestory Mjunangoma tukio lilifanyika Wilayani kwimba.

Msanifu Majengo kutoka TBA, Bi. Suzanne Boniphace akikabidhi hati ya makabidhiano ya jengo la Mahakama ya Wilaya Kwimba kwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Nestory Mjunangoma katika tukio la makabidhiano ya jengo la Mahakama ya wilaya kwimba lililofanyika mjini Ngudu.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika tukio la makabidhiano ya jengo la Mahakama ya Wilaya Kwimba wilayani wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jengo hilo, wa kwanza kulia ni Mhe Dastani Ndeko, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya wilaya Kwimba Mhe. Dastan Ndeko, Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza Bw. Nestory Mjunangoma (wa pili kulia), Bi Sarai Semkuyu kutoka Mahakama Kuu Mwanza (katikati) na Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Kwimba Bi. Origa Kosani.

Msanifu Majengo kutoka TBA Bi. Suzanne Boniphace akizungumza jambo wakati wa kikao cha makabidhiano ya jengo la Mahakama ya Wilaya Kwimba jana tarehe 30 Oktoba, 2023 tukio lilifanyika katika Mahakama ya wazi ya Wilaya ya Kwimba. Katikati ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Bw Nestory Mjunangoma akifuatiwa na kulia mwenye nguo nyeusi ni Mhandisi kutoka Kampuni ya Uhandisi ya Kiure Bw. Mbezi Sumai Mhandisi

Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya wilaya Kwimba lililokabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania jana tarehe 30 Oktoba 2023, tukio lilifanyika mjini Ngudu na kuhudhuliwa na watumishi mbalimbali wa Mahakama na wananchi wa Kwimba (hawapo pichani).

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Ngudu Mjini ambalo lilikuwa likitumiwa na Mahakama ya Wilaya Kwimba kutolea huduma kwa wananchi kabla ya kukabidhiwa kwa jengo jipya la kisasa.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni