Na. James Kapele- Mahakama, Katavi
Kaimu Mkuu wa Gereza la
Mahabusu Mkoa wa Katavi, Kamishina Msaidizi wa Magereza (ACP) Christopher Fungo
ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kusimika mfumo mzuri na bora wa usikilizaji
wa mashauri kwa njia ya mtandao.
Mfumo huo utawezesha
kusikilizwa mashauri kwa njia ya mtandao bila kumtaka mshitakiwa kufika
mahakamani, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za gereza hilo.
Vifaa hivyo ambavyo ni TV
na vifaa vingine wezeshi kutoka Mahakama ya Tanzania viliwasilisha gerezani
hapo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway
Sumaye.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Kaimu Mkuu wa Gereza hilo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuona
umuhimu wa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitawezesha na kuongeza ufanisi katika
usikilizaji wa mashauri.
“Kwa hakika vifaa hivi
vimeletwa kwa wakati ambao vinahitajika sana kwa kuwa Mkoa huu una gereza moja
tu la mahabusu ambao huletwa hapa kutoka katika Wilaya zote. Hivyo niishukuru
sana Mahakama kwa kuwa vifaa hivi vitasaidia kutupunguzia gharama za uendeshaji
wa mashauri, hasa ukizingatia jiografia ya Mkoa wetu,” alisema.
Vifaa hivyo vimesimikwa
na Afisa Tehama wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bw. Innocent Mayanga ambaye
amewapitisha baadhi ya askari magereza wanaosimamia gereza hilo matumiziya
mfumo huo.
Awali, akikabidhi vifaa
hivyo, Mhe Sumaye amewahimiza askali hao kuvitunza kwa kuwa vimepatikana kwa
gharama kubwa na kwamba vitasaidia katika uendeshaji wa mashauri.
Upatikanaji wa vifaa
hivyo kwa magereza ni moja katika ya mipango mahsusi ambayo Mahakama imejiwekea
katika mpango mkakati wa kuboresha huduma ili kuhakikisha mashauri yote
yanasikilizwa kwa wakati.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe, Gway Sumaye (wa tatu kutoka kulia) akikabidhi vifaa hivyo kwa Kaimu Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mpanda. Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Katavi, Bw. Allan Mwella (wa pili kushoto) ambaye naye alishiriki shughuli hiyo.
Sehemu ya wafungwa wakiingiza vifaa hivyo gerezani kwa ajili ya kusimikwa rasmi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni