Jumanne, 31 Oktoba 2023

WADAU WANA MCHANGO MKUBWA KUONDOA, KUZUIA MASHAURI YA MLUNDIKANO: JAJI MANSOOR

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor amewapongeza wadau wote wa Mahakama kwa mchango wao mkubwa katika kuondoa mashauri ya mlundikano.

Mhe. Mansoor alitoa pongezi hizo wakati wa vikao vya kusukuma mashauri ya jinai na madai vilivyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo mkoani hapa.

“Hili ni jambo la kujivunia kuwa Kanda yetu ya Morogoro hakuna kesi za mlundikano, hongereni sana kwa wadau wetu maana mngetukwamisha tusingeweza kuyafikia haya mafanikio, juhudi zenu zinafahamika” alisema.

Mhe. Mansoor aliongeza kuwa watumishi wa Mahakama wote kwa umoja wao wamechangia pia katika kufikia mafanikio hayo.

Kauli hiyo ya Jaji Mfawidhi iliungwa mkono na Jaji wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Gabriel Malata ambaye alisema timu hiyo ya wadau wa Mahakama ni ya ushindi ambayo haipaswi kurudi nyuma katika zoezi zima la utoaji haki.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando alieleza hali ya mashauri kwa upande wa Mahakama Kuu kwa kipindi cha mwezi Julai hadi tarehe 26 Oktoba, 2023.

Alieleza kuwa mashauri ya madai yaliyofunguliwa kwa kipindi hicho yalikuwa 218, yaliyomalizika ni 270 na yaliyobakia na yanaendelea kusikiliza ni mashauri 254.

Kwa upande wa mashauri ya jinai, Mhe. Mmbando alieleza kuwa kuanzia Julai hadi 27 Oktoba, 2023 yalifunguliwa 182, yaliyosikilizwa ni 191 na yaliyobakia ni 80. Alisema kwa sasa hakuna mashauri ya mlundikano na hawategemei kuwa nayo katika kituo hicho.

Naibu Msajili alitumia fursa hiyo kuwajulisha wadau juu ya matumizi ya mfumo mpya wa usajili wa mashauri (e-CMs) ambao ni maboresho ya mfumo wa JSDS2 na kuongeza kuwa kwa sasa mfumo huo upo kwenye majaribio.

Alisema kuwa hivi punde mfumo huo mpya utaanza kutumika kikamilifu, hivyo aliwahimiza kufanya jitihada za kujifunza na kuujua mfumo huo.

“Rai yetu wadau wetu wote kuendelea kuzingatia matumizi ya mifumo hii, pia nitoe pongezi za dhati kwa wadau wetu wanaokwenda sambamba na kasi yetu ya uendeshaji na usikilizaji wa mashauri” alihitimisha Mhe. Mmbando.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kwa Kanda ya Morogoro, Msomi Baraka Lweeka aliipongeza Mahakama kwa kupiga hatua kubwa na kwa ushirikiano mzuri wanaoupata, hivyo kuchochea mashauri humalizika kwa wakati.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor akiendesha vikao vya kusukuma mashauri vilivyofanyika hivi karibuni.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata akifuatilia taarifa iliyokuwa ikisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando (hayupo pichani).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando akiwapitisha wajumbe wa kikao kwenye taarifa ya mashauri wakati wa vikao vya kusukuma mashauri.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akifuatilia jambo wakati wa kikao.

Bi. Neema Haule kutoka Ofisa ya Taifa ya Mashtaka Morogoro akichangia mada wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya wajumbe wakati wa kikao wakifuatilia masuala mbalimbali.

Wajumbe wa kikao ambao pia ni Wenyeviti wa Mabalaza ya Ardhi Morogoro wakifuatilia mjadala wakati wa kikao.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, Bi. Elinuru Maleko akifuatilia mijadala ndani ya kikao cha kusukuma mashauri.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni