Jumatatu, 30 Oktoba 2023

JMAT TAWI LA KAGERA YAFANYA KIKAO; JAJI BANZI AWASISITIZA KUKUTANA MARA KWA MARA

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambaye pia ni Mwenyekiti na Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Kagera, Mhe. Immaculata Banzi amewasisitiza Viongozi wa Chama hicho mkoani humo kuhakikisha Mahakimu wanakutana mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto mbalimbali za kikazi.

Akizungumza hivi karibuni na Viongozi na Wajumbe wa Chama hicho mkoani humo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Banzi alisema vikao hivyo ni muhimu kwani   vinawaleta pamoja Majaji na Mahakimu.

“Niwasisitize Viongozi wa JMAT kuhakikisha Mahakimu wanakutana na kubadilishana uzoefu, vikao hivi ni muhimu kwani vinaleta Mahakimu pamoja na kujadiliana masuala ya kazi pamoja na changamoto zao,” alisema Mhe. Banzi.

Mhe. Banzi aliongeza kwa kusema, “Mtakumbuka mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2023 tulipokea ugeni wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwenye Kanda yetu na ugeni huo uliongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Juma, Tume ilitoa pongezi sana kwa Kanda yetu kwa kasi nzuri ya usikilizwaji wa mashauri hivyo naomba kufikisha pongezi hizo kwenu pia” a.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa JMAT tawi la Kagera, Mhe. Edward Samara aliwaomba wajumbe kuendelea na utoaji wa michango ya kila mwezi. Kwa kuwa michango hiyo inasaidia sana uendeshwaji wa shughuli za tawi hilo pamoja na kuwakaribisha wajumbe wapya kwenye tawi hilo.

Katika kikao hicho, wanachama waliwasilishiwa taarifa ya michango yao ambapo, Mweka hazina wa Tawi hilo, Mhe. Erasto Joseph aliwaomba wasiokamilisha michango yao kukamilisha kwa wakati.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambaye pia ni Mwenyekiti na Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Kagera,  Mhe. Immaculata Banzi (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha JMAT Tawi la Kagera. Kulia ni Makamu Mwenyeki-JMAT, Mhe. Edward Samara na kushoto ni Katibu JMAT Kagera, Mhe. Zakaria Nyahende.
Makamu Mwenyekiti JMAT Kagera, Mhe. Edward Samara aliyesimama akifafanua jambo wakati wa  kikao cha JMAT Tawi la Kagera.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Emmanuel Ngigwana (katikati)  akichangia mada. Pamoja naye ni wanachama wa JMAT Kagera.
Msaidizi wa  Sheria wa  Jaji  Hakimu Mwandamizi, Mhe. Edwin Kamaleki ambaye akiwasilisha mada iliyohusu 'Common Mistakes done in Court.'
Wajumbe wakimsikiza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambaye pia ni Mwenyekiti na Mlezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Kagera, Mhe. Immaculata Banzi (hayupo katika picha).

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni