Jumapili, 29 Oktoba 2023

MKUTANO MKUU SEACJF WAHITIMISHWA KWA MAFANIKIO; MAJAJI WAKUU WAELEZA WALIVYOFURAHISHWA

Na Mary Gwera, Mahakama

Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJ), wametoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania na Uongozi wa Mahakama nchini kwa kuandaa vema Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa hilo uliomalizika hivi karibuni na kusema kuwa maandalizi yaliyofanyika ni mfano wa kuigwa kwa Mahakama nyingine za Ukanda huo.

Akizungumza katika mahojiano maalum tarehe 26 Oktoba, 2023 katika Hoteli ya ‘Mount’ Meru jijini Arusha, Jaji Mkuu wa Namibia na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo aliyemaliza muda wake, Mhe. Peter Shivute alisema kuwa, Mkutano huo ulioanza tarehe 23 Oktoba mwaka huu ulienda vizuri.

“Ninayo furaha kuwa mkutano wa mwaka huu uliofanyika nchini Tanzania ulienda vizuri sana, mipangilio ilikuwa mizuri sana vilevile tunashukuru sana kwa ukarimu ulioonyeshwa kwetu, Mahakama ya Tanzania imeweka mfano ambao ni muhimu kuigwa kwa Mahakama nyingine,” alisema Mhe. Shivute.

Mhe. Shivute alimshukuru pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga muda wake na kufungua Mkutano huo muhimu ambao anakiri kuwa walithamini na kufurahishwa na kitendo hicho.

Aidha, Mhe. Shivute alikiri wazi kuwa, huu ni moja kati ya mikutano ambao ulihudhuriwa na idadi kubwa zaidi ya Majaji Wakuu Wanachama ambapo anasema kuwa waliohudhuria walikuwa 15 kati ya 16 na kusema kwamba, idadi hiyo imevunja rekodi nah ii imetokana pia na ushawishi wa Mahakama, mada zilizopangwa ikiwa ni pamoja na kaulimbiu ya mwaka huu ambayo kwake anasema imekuwa kivutio.

Akizungumzia kuhusu idadi ya Wanachama wa Jukwaa hilo, Jaji Mkuu huyo alitoa rai kwa Majaji Wakuu ambao nchi zao zipo Kusini na Mashariki mwa Afrika kujiunga na SEACJF ili kuongeza nguvu katika masuala ya maendeleo ya Mahakama za barani Afrika.

“Bado hatujaridhika na idadi ya wanachama tulionao, Jukwaa hili litakuwa bora kama Majaji Wakuu wa nchi zote zinazohusika watafanikiwa kujiunga, hivyo tunaendelea kuwakaribisha kujiunga kwa sababu ni vizuri kwetu sisi wote kama Mahakama za bara la Afrika kuwa na kiwango kimoja cha maendeleo katika Uhuru na kanuni zote zinazoathiri Mahakama,” alisema Mhe. Shivute.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Kenya, Mhe. Martha Koome pamoja na kusisitiza Majaji Wakuu kuendelea kujiunga na Jukwaa hilo ili kuwa na sauti ya pamoja, ameishukuru Tanzania kwa ukarimu waliouonesha kwao kwa kipindi waliokuwa hapo. 

Aidha, Mhe. Koome aliongeza kuwa, alivutiwa na majadiliano kuhusu utatuzi wa migogoro katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, matumizi ya Teknolojia katika utoaji wa haki pamoja na uamuzi wa utatuzi wa migogoro katika maeneo yao ambazo ni mada muhimu katika uendeshaji wa Mahakama za nchi wanachama.

“Mkutano huu umetuwezesha kukaa pamoja na kujadili masuala mbalimbali, mfano katika matumizi ya teknolojia, tumeweza kuona Tanzania imefika mbali kwa kuingiza matumizi ya akili bandia hasa kwenye kutafsiri mashauri, hivyo imetuwezesha na sisi kufahamu zaidi matumizi ya teknolojia,” alisema Mhe. Koome. 

Aliongeza kwamba, katika Mkutano huo walipata nafasi ya kuzungumzia changamoto za Mahakama zao ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya jinsi wanavyoweza kusaidia watu kupata haki zao mapema kwani watu wa nchi zote wako sawa na mahitaji yao ni sawa na wote wanahitaji kupata haki kwa wakati.

Katika Mkutano huo mada mbalimbali zilitolewa na majadiliano yalifanyika yote yakilenga kuboresha huduma ya utoaji haki katika Nchi Wanachama wa Jukwaa hilo.

Kaulimbiu ya Mkutano huo kwa mwaka huu ni; Wajibu wa Mahakama za Kitaifa katika utatuzi wa Migogoro kwenye Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA): Matumizi ya Teknolojia ya Kisasa ili kuongeza  Ufanisi Katika Utoaji Haki.

Kaulimbiu hii inalenga kurahisisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo. Hii ni pamoja na kuhakikisha zinakuwepo Sheria mbalimbali zitakazowezesha ufanyaji biashara baina ya nchi za Ukanda wa Afrika, kusikiliza na kutatua migogoro ya biashara kisheria na hatimaye kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi hizi kutokana na ukweli kwamba wafanyabiashara watafanya kazi zao kwa wepesi zaidi.  

Katika kutambua na kukuza jukumu muhimu la Mahakama ndani ya Kanda, Majaji Wakuu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika waliamua kuanzisha Jukwaa mwaka 2003 ili, pamoja na mambo mengine, kuzingatia Utawala wa Sheria, Demokrasia, Uhuru wa Mahakama na kukuza mawasiliano ya pamoja.

Maono au mtazamo wa Jukwaa hilo ni kuwa na Mahakama iliyobadilika, iliyo huru, iliyounganishwa na yenye umoja ambayo inakuza utawala wa sheria, haki, demokrasia na utawala bora ili kuhakikisha ustawi, usawa, amani na usalama wa raia wote.

Jaji Mkuu wa Namibia na Mwenyekiti wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) aliyemaliza muda wake punde, Mhe. Peter Shivute (aliyeketi mbele) pamoja na Majaji Wakuu wengine wa Jukwaa hilo wakiwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka (AGM) wa Jukwaa hilo uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.
Jaji Mkuu wa Namibia na Mwenyekiti wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) aliyemaliza muda wake, Mhe. Peter Shivute akiwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa SEACJF uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha.

Jaji Mkuu wa Kenya na Rais wa Mahakama ya Juu nchini humo, Mhe. Martha Koome akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika jijini Arusha hivi karibuni.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni