Jumatatu, 23 Oktoba 2023

PROF. JUMA ATOA USHAURI MUHIMU KWA MAJAJI WAKUU AFRIKA

Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) kuitafakari kwa kina Kaulimbiu ya Mkutano wa mwaka huu inayohimiza wajibu wa Mahakama katika utatuzi wa migogoro kwenye eneo huru la biashara sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Akizungumza leo tarehe 23 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa ‘Mount’ Meru jijini Arusha, wakati akitoa neno la ukaribisho kwa Majaji Wakuu hao pamoja na wageni wengine waliohudhuria katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo uliofanywa na Rais Samia, Mhe. Prof. Juma amesema ni muhimu nchi hizo kuzingatia ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Kuhusu eneo la Biashara huria ambalo pia lipo katika kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu linaweza kuonekana kuwa mbali kwa Mahakama zetu za kitaifa lakini eneo hili kwa uhalisia ni jambo la kweli, hivyo yatupasa kutafakari juu ya matarajio ya Mahakama zetu kuhusu eneo hili,” amesema Prof. Juma.

Amesema, Mkutano huu ambao hufanyika kila mwaka huzipa Mahakama za Kitaifa majukwaa ya ushirikiano ambapo hukutana ili kujadili baadhi ya mambo mapya yanayokabili usimamizi wa haki katika mamlaka mbalimbali za Mahakama katika Nchi Wanachama.

Kwa upande wa matumizi ya Teknolojia, Jaji Mkuu amesema katika Dunia ya leo matumizi ya teknolojia hayaepukiki, hivyo hata katika masuala ya kisheria teknolojia ni lazima, ameongeza kwa kutoa mfano kwamba, wakati wa UVIKO 19, Mahakama ya Tanzania haikusimamisha shughuli zake bali iliendelea kusikiliza mashauri kwa njia ya TEHAMA. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), Mhe. Peter Shivute amesema Jukwaa hilo ni fursa ya kujadili mada mbalimbali na kufahamu changamoto wanazokabiliana na namna ya kuzitatua.

Kwa mujibu wa Mhe. Shivute, ambaye ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Namibia, mpaka sasa Jukwaa hilo lina wanachama 16 ambapo katika mkutano huu umehudhuriwa na wanachama 15.

Mkutano huu hufanyika kila mwaka na awamu hii ni mara ya kwanza kufanyika nchini Tanzania. Jukwaa hili lilianzishwa tarehe 07 Desemba, 2003, Johannesburg nchini Afrika Kusini. 

Jukwaa hilo lilianzishwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na kukuza Utawala wa Sheria, Demokrasia na Uhuru wa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) (hawapo katika picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa hilo uliofanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2023 katika Ukumbi wa mikutano wa 'Mount' Meru jijini Arusha.
Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF (walioketi mbele) pamoja na wageni wengine wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa hilo leo tarehe 23 Oktoba, 2023.

Jaji Mkuu wa Namibia na Mwenyekiti wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF) akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jukwaa hilo.

Sehemu ya wageni wakifuatilia yanayojiri katika Mkutano huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki Mwa Afrika kabla ya Mkutano wa Jukwaa la Majaji hao uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha leo tarehe 23 Oktoba, 2023.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni